• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Corona: Hitilafu ya oksijeni hospitalini yaua watatu

Corona: Hitilafu ya oksijeni hospitalini yaua watatu

Na ERIC MATARA

WATU watatu waliokuwa wakiugua Covid-19 walifariki katika Hospitali ya Nakuru Level Five, baada ya hitilafu kutokea katika kiwanda kidogo cha kutengeza oksijeni hospitalini humo.

Watatu hao, ambao walikuwa wakiongezwa oksijeni ya ziada katika hospitali hiyo kubwa zaidi Kusini mwa Rift Valley, walifariki mwishoni mwa wiki iliyopita.

Ilibianika kuwa vifo hivyo vilitokea kutokana na hitilafu katika kitengo cha oksijeni kilichoko katika hospitali hiyo.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Nakuru, Dkt Gichuki Kariuki, alithibitisha vifo hivyo.

“Ni kweli kwamba tumewapoteza wagonjwa watatu, ambao walikuwa wakiongezewa oksijeni katika Hospitali ya Nakuru Level Five. Kiwanda cha oksijeni kilipata hitilafu Jumamosi na kuchangia uhaba. Hitilafu hiyo ya kiufundi ilidumu kwa karibu saa nne,” akasema Dkt Gichuki.

“Kutokana na hitilafu hiyo ya kiufundi, kiwanda cha oksijeni kilifeli kuzalisha mitungi 80 ya hewa hiyo. Kilizalisha mitungi 40 na kusababisha uhaba wa mitungi 40. Hata hivyo, tuliweza kupokea mitungi ya oksijeni kutoka Nairobi na Eldoreti. Wagonjwa wengi wangefariki ikiwa maafisa wa afya hawangechukua hatua za haraka,” akaeleza Dkt Kariuki.

Vifo hivyo, vilitokea wakati kiwanda cha oksijeni katika hospitali hiyo kimelemewa kutokana na ongezeko la hitaji la hewa hiyo wakati huu ambapo kaunti hiyo inaandikisha idadi ya juu ya maambukizi.

Hospitali hiyo ya rufaa huhudumia kaunti ya Nakuru na kaunti jirani za Baringo, Samburu, Kericho, Narok, Nyandarua na Bomet.

Vifo hivyo, vimejiri wakati serikali ya Kaunti ya Nakuru inakabiliwa na shinikizo za kupambana na ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19.

Gavana Lee Kinyanjui wiki iliyopita alifichua kuwa kuna uhaba wa vitanda katika vitengo vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICUs) katika kaunti hiyo.

Kufikia jana, jumla ya wagonjwa 74 wa corona walikuwa wakiongezwa oksijeni ya ziada katika hospitali mbalimbali katika kaunti ya Nakuru. Wengine wanne walikuwa wakihudumiwa katika ICU.

Kufikia jana, Nakuru imeandikisha jumla ya visa 7,429 vya corona tangu Machi 30, 2020, kaunti hiyo iliponakili kisa cha kwanza cha Covid-19.

Vile vile, kaunti ya Nakuru imerekodi vifo 211 kutokana na ugonjwa huo tangu mwaka jana.

You can share this post!

Nyoro ajadiliana na madiwani jinsi ya kufufua miradi...

Wizara yamtishia mwalimu aliyefichua masaibu yake