• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 12:38 PM
ODM yataka msajili atatue mzozo wa fedha wa NASA

ODM yataka msajili atatue mzozo wa fedha wa NASA

Na MWANDISHI WETU

CHAMA cha ODM, sasa kinataka msajili wa vyama vya kisiasa kutatua mzozo wa fedha kati ya chama hicho na vyama tanzu vya muungano wa NASA.

Vyama vya Wiper, Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya vimekuwa vikilaumu ODM kwa kukataa kuvigawia pesa kutoka hazina ya vyama vya kisiasa kinyume na mkataba wa muungano huo.

ODM imekuwa ikikanusha madai hayo na sasa imemwandikia barua msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu kumuomba aitishe mkutano kati ya vyama hivyo kusuluhisha suala hilo.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna anataja madai ya vyama hivyo kama uongo kwa kuwa kuna mkataba uliowasilishwa kwa msajili wa vyama unaoweka wazi makubaliano yaliyoafikiwa na vyama tanzu vya NASA.

“Msimamo wetu ni kwamba NASA sio shirika la siri lakini muungano uliosajiliwa na msajili wa vyama vya kisiasa na unaoongozwa na mkataba uliowekwa katika ofisi yake, ambao yaliyomo yanaeleweka bayana,” alisema Bw Sifuna kwenye barua yake kwa Bi Nderitu.

“Kwa hivyo, tunaomba ofisi yako kuitisha mkutano haraka iwezekanavyo wa vyama tanzu vya NASA alivyoomba Bw Musyoka ili kujadili na kusuluhisha suala hili kabisa,” anaomba Bw Sifuna.

Mnamo Aprili, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka aliandikia msajili wa vyama vya kisiasa kuhusu suala hilo.

Bw Musyoka na Bw Mudavadi wamekuwa wakilaumu ODM, inayoongozwa na Bw Raila Odinga, kwa kusaliti washirika wake katika NASA wakidai walikataa kugawana pesa hizo na nyadhifa za uongozi bungeni.

Juhudi za kupatanisha vinara wa muungano huo zinaendelea huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia. Wiki jana, Bw Musyoka aliashiria kuwa alikutana na Bw Odinga kujadili suala hilo na fedha lakini akaongeza hawakujadili uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Odinga amekuwa akikanusha madai ya vinara wenzake akisema kwamba chama chake kinapokea pesa kwa kutegemea idadi ya wabunge wake na kwamba hakingekataa kuwapa washirika wake haki yao.

“Kuna wanaosambaza uvumi kwamba ODM inanyima washirika wake pesa. Kama pesa ziko, tutawapa,” alisema akihojiwa na Radio Citizen mapema wiki hii.

You can share this post!

Waiguru ahisi huu ni wakati mwafaka wa Jubilee kuzinduka

Waziri atangaza Sikukuu Jumanne Waislamu wakiadhimisha...