• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Polisi walaumiwa kwa kufumbia macho masaibu ya wasichana wa shule wanaonyemelewa kila uchao

Polisi walaumiwa kwa kufumbia macho masaibu ya wasichana wa shule wanaonyemelewa kila uchao

NA MWANDISHI WETU

MAAFISA wa polisi mjini Kilifi wanalaumiwa kwa kufumbia macho masaibu ya wasichana wa shule wanaonyemelewa na wabakaji kila uchao.

Visa vya wasichana kudhulumiwa kingono vinaongezeka mjini humo na hata polisi mmoja mjini Kilifi anadaiwa kumbaka mwanafunzi wa Kidato cha Nne kutoka shule moja ya upili katika eneobunge la Kilifi Kaskazini mnamo Jumatatu, Juni 5, 2023. Inadaiwa kwamba afisa huyo alitekeleza unyama huo saa kumi asubuhi.

Mwanafunzi huyo, ambaye wazazi wake wanasema alifanyiwa operesheni mnamo Januari 2023 na anaendelea kupokea matibabu, alikuwa ametoka katika nyumba aliyokodishiwa akielekea shuleni kuchukua vitabu vya kudurusu maana alikuwa mgonjwa.

Ghafla gari la polisi lilisimama na dereva akamuuliza alikokuwa akielekea alfajiri hiyo.

Afisa huyo ni dereva katika makao makuu ya polisi mjini Kilifi. Afisa huyo pia anakabiliwa na tuhuma nyingine za kumbaka na kumpachika mimba msichana ambaye alikuwa hajafikisha umri wa utu uzima.

Kufuatia changamoto za kifedha miongoni mwa familia nyingi katika Kaunti ya Kilifi, hali ambayo imechangiwa na umaskini mkubwa, wanafunzi wengi wa shule za upili hukodishiwa na wazazi wao nyumba za kuishi karibu na shule za kutwa ili kuwapunguzia mwendo mrefu kusafiri kila siku.

Akizungumza na Taifa Leo, mwanafunzi huyo ambaye tayari ni mtu mzima kwa sababu kisheria yuko katika kategoria ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi, alisema afisa huyo wa polisi alimwamrisha aabiri gari hilo kwani.

Inadaiwa kwamba afisa huyo alisema angempeleka katika kituo cha polisi ila akampeleka nyumbani mjini Kilifi ambapo alimlazimisha wafanye mapenzi na kumpa nauli kurudi kwake.

“Polisi huyo alikuwa mkali kwangu na kuniambia kuwa ilikuwa hatia kwa mtu yeyote kutembea alfajiri mbichi kama siku hiyo. Aliniamuru niabiri kwenye gari hilo la polisi kwani alikuwa amenitia mbaroni na angenipeleka kwenye kituo cha polisi,” akaeleza.

Alipoingia kwenye gari hilo, afisa huyo alifululiza hadi kwenye lango la kituo cha polisi cha Matsangoni lakini hakuingia ndani ya kituo.

Alimweleza mwanafunzi huyo ya kwamba alikuwa amebadilisha nia na hangemtia mbaroni bora tu afuate masharti yake.

Walianza safari ya kuelekea Kilifi na kila mara walipokariia kwenye taa za barabarani, afisa huyo wa polisi alimwamrisha kujificha ili asionekane.

“Kulipopambauka kabisa alinipa pesa nitumie kama nauli na kusema kuwa hangenirudisha aliponitoa kwa sababu gari hilo la polisi halikustahili kuwa kwake hadi muda huo,” akasema mwanafunzi huyo.

Pia alimwambia abadilishe nguo aliyokuwa amevaa na badala yake akampa suruali ndefu.

Taifa Leo imethibitsha ya kwamba mwanafunzi huyo alitambua nyumba ya afisa huyo wa polisi mnamo Jumanne wiki jana.

Gwaride la kumtambua askari huyo lilifanyika katika katika kituo cha polisi cha Kilifi mnamo Alhamisi wiki jana.

Familia ya mwathiriwa imetoa wito kwa watetezi wa haki, serikali na idara husika kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha mtoto wao anapata haki.

Babake mwathiriwa amesema kuwa amekuwa akipigiwa simu kutoka kwa watu wengi wakimtaka kutupilia mali kesi hiyo ya mwanawe.

Alisema kuwa watu hao walisema kuwa kesi hiyo ingefanya afisa huyo wa polisi kupoteza kazi.

“Mwanangu analilia haki na ombi langu kwa serikali ni ihakikishe kuwa anapewa haki hiyo,” akasema.

Naye kakake mwathiriwa anaeleza masikitiko yake kuwa afisa huyo wa polisi alimdhulumu mwanafunzi huyo. Anaitaka Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi [IPOA] kuichukulia kwa uzito kesi hiyo na kuhakikisha mwathiriwa anapata haki.

“Polisi wanaendeleza uchunguzi na wito wetu ni kwamba serikali na asasi husika itahakikisha ya kwamba haki inatendeka,” akasema kaka ya mwathiriwa.

Anasema dadake alianza safari ya kutafuta haki bila kusukumwa na mtu yetote na wao kama familia wako nyuma yake.

Baada ya kupitia dhuluma ya ngono, mwathiriwa alimweleza rafiki yake ambaye alimshauri kwenda hospitalini na kisha kupiga ripoti katika kituo cha polisi. Rafiki yake huyo naye alidai polisi aliwahi kujaribu kumdhulumu lakini akaokolewa na ndugu zake waliomtisha afisa.

Aliomba ruhusa kwa mwalimu wake wa darasa na akaenda katika kituo cha afya cha Matsangoni kwa matibabu, kisha akapiga ripoti katika kituo cha polisi cha Matsangoni ambapo walimwelekeza katika kituo cha polisi cha Kilifi.

Juhudi za kupata ripoti kutoka kwa polisi hazikufua dafu kwani kamanda wa polisi wa kaunti Kilifi Bi Fatuma Hadi hakupokea simu wala kujibu ujumbe wa arafa.

  • Tags

You can share this post!

Majanajike wanajeshi wa ukombozi

Eric Omondi aenda Uingereza na kugeuka ombaomba barabarani,...

T L