• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Polisi wavunja kufuli kusaidia Spika

Polisi wavunja kufuli kusaidia Spika

Na WYCLIFFE NYABERI

POLISI jana walilazimika kuvunja makufuli yaliyotumiwa kulifunga lango la watu mashuhuri kwenye majengo makuu ya kaunti ya Kisii, ili kumruhusu Spika wa bunge la kaunti hiyo Bw David Kombo kuingia kazini.

Bw Kombo anayekabiliwa na masaibu chungu nzima kufuatia jaribio la kumng’atua mamlakani, aliwasili mapema kama siku zingine kuongoza shughuli katika bunge hilo lakini akakwama nje kwa kuwa hakuna bawabu yeyote aliyejitokeza kumfungulia.

Inasemekana baadhi ya MCAs ambao wamekuwa wakishinikiza aondoke afisini, ndio waliochangia kufungwa kwa lango hilo baada ya kupata habari kwamba Bw Kombo alikuwa na nia ya kuongoza kikao cha asubuhi.

Katika siku za hivi karibuni, hakujawahi kuwa na utulivu wala biashara zozote zinazofanyika katika bunge la kaunti ya Kisii kufuatia mvutano uliopo baina ya mirengo miwili ya madiwani.Mrengo mmoja unadai kwamba Bw Kombo aling’atuliwa mamlakani kwa kura waliyoipiga huku mwingine ukishikilia kuwa kigezo cha kumwondoa afisini Spika huyo hakikutimizwa kikatiba.

Kutokana na ubishi huo, Spika Kombo alielekea mahakamani alikopata afueni ya kumruhusu ahudumu kwenye wadhfa wake hadi kesi aliyoiwasilisha isikizwe na kuamuliwa.Hata hivyo, wanaompinga waliapa kutompa wakati rahisi kuwaongoza na hivyo basi kumwekea vikwazo vya kumuzuia aingie bungeni.

Licha ya kasheshe hizo, maafisa wa polisi walimsaidia Bw Kombo kuingia bungeni ambako alihudhuria kikao na madiwani watano wanaomuunga mkono. Kwa kuwa nambari hiyo ya madiwani ilikuwa ya chini mno, alilazimika kuahirisha kikao hicho na kuwaomba MCAs wote washirikiane naye.

  • Tags

You can share this post!

Wavuvi washauriwa wawe waangalifu msimu wa mvua

Ni makosa kulazimishia Wakenya vyama vya kisiasa