• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wavuvi washauriwa wawe waangalifu msimu wa mvua

Wavuvi washauriwa wawe waangalifu msimu wa mvua

Na KALUME KAZUNGU

MABAHARIA na wavuvi, katika Kaunti ya Lamu wameonywa dhidi ya kutumia njia hatari ndani ya Bahari Hindi wakati huu ambapo eneo la Pwani linashuhudia mvua kubwa.

Baadhi ya njia hatari za baharini zinazotambulika Lamu hasa kutokana na mawimbi yake makali na dhoruba ni Mlango wa Tanu ulioko eneo la Mkokoni, Mlango wa Ali ulioko Kipungani, Mlango wa Bomani ulioko Kiunga, Mlango wa Shella, Manda Bruno na kivuko cha Mkanda.

Katika mahojiano na Taifa Leo jana, Afisa wa Idara ya Hali ya Hewa, Kaunti ya Lamu, Edward Ngure, alisema ni vyema ikiwa mabaharia na wavuvi wataepuka kutumia sehemu hizo kwa muda hadi pale mvua na upepo ambao umekuwa ukishuhudiwa utakapopungua.

“Si vyema wakati mvua inaponyesha wavuvi na mabaharia wetu kuendelea kutumia njia hatari, ambapo ajali za boti au mashua zao zinapotokea inakuwa vigumu kuwaokoa,” akasema Bw Ngure. Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Kitengo cha Kuokoa wakati wa Majanga, Kaunti ya Lamu, Luqman Abdulaziz, alisema ipo haja ya mabaharia na wavuvi kuchukua tahadhari na maonyo yote yanayotolewa na idara ya hali ya anga kwa uzingativu ili kusiwe na ajali na maafa baharini.

kamailivyokuwa ikishuhudiwa miezi ya awali.“Tunashukuru kwamba miezi zaidi ya mitano sasa imepita bila kushuhudia mkasa wa ajali baharini. Ni vyema wanaotumia baharini kutilia maanani maonyo ya idara ya hali ya anga hasa msimu huu wa mvua ili wasipate shida baharini,” akasema Bw Abdulaziz.

Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Baharini, Kaunti ya Lamu, Hassan Awadh aliwashauri manahodha wa boti na mashua kuhakikisha wanatundika taa zao za mbele wanapoendesha vyombo vyao baharini ili waweze kutambuliwa na wenzao na kuepuka kugongana wanaposafiri baharini nyakati za alfajiri, usiku au msimu wa mvua ambapo huwa kuna ukungu na giza.

  • Tags

You can share this post!

Fahamu nani atakutana na nani kwenye droo kali ya hatua ya...

Polisi wavunja kufuli kusaidia Spika