• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Pwani yapata uhaba wa samaki licha ya kuwa jirani wa bahari

Pwani yapata uhaba wa samaki licha ya kuwa jirani wa bahari

Na ANTHONY KITIMO

UKANDA wa Pwani hupoteza zaidi ya Sh45 bilioni kila mwaka kwa sababu ya kiwango cha chini cha uvuvi licha ya kuwa jirani wa Bahari Hindi.

Taasisi ya Utafiti wa Baharini na Uvuvi (KeMFRI) inasema kuwa uvuvi unaofanywa Pwani hunasa chini ya asilimia 10 ya samaki, ikilinganishwa na kiwango kinachoweza kupatikana kukiwa na uwekezaji bora katika sekta hiyo.Kulingana na taasisi hiyo, Kenya hutegemea zaidi samaki kutoka Ziwa Victoria.

Ziwa hilo limekumbwa na uhaba katika miaka ya hivi majuzi, na hivyo kufungua soko la nchi kwa uagizaji samaki kutoka nchi za nje kama vile China.Mkurugenzi Mkuu wa KEMFRI, Prof James Njiru, alisema licha ya kuwa Bahari Hindi ina zaidi ya aina 10 za samaki, kiwango kinachovuliwa ni kidogo mno.

“Kwa sasa huwa tunapata takriban Sh5 bilioni kwa uvuvi katika Bahari Hindi lakini kukiwa na uwekezaji bora, tunaweza kupata zaidi ya Sh50 bilioni kutoka kwa ukanda wa Pwani pekee,” akasema Prof Njiru.

Akizungumza katika eneo la Gasi, Kaunti ya Kwale wakati wa kuadhimisha Siku ya Bahari Ulimwenguni, Prof Njiru alisema takriban tani 120,000 za samaki zinazouzwa nchini huvuliwa kutoka Ziwa Victoria. wa upande mwingine, tani 26,000 pekee ndizo huvuliwa Pwani.

Alieleza matumaini kuwa ukarabati wa kiwanda cha samaki cha Liwatoni, Mombasa utasaidia kuvutia wawekezaji wengi kwa sekta ya uvuvi. Kwa sasa, Kenya haina wataalamu wa hali ya juu wanaoweza kufanya shughuli za uvuvi katika kina kikuu cha maji baharini.

na hulazimika kuajiri watu kutoka nchi za kigeni.Vile vile, aina hiyo ya uvuvi hutegemea vyombo na vifaa kutoka mataifa ya nje kwani havipatikani kwa urahisi humu nchini.Katika mahojiano ya awali, Waziri wa Kilimo na Uvuvi, Bw Peter Munya alisema serikali ilikuwa imetenga Sh5 bilioni kustawisha sekta ya uvuvi.

Ukarabati tayari ulianzishwa katika fuo za uvuvi Vanga, Kibuyuni na Gazi (Kaunti ya Kwale), Ngomeni na Kichwa cha Kati (Kaunti ya Kilifi).Fuo hizo zinatarajiwa kusambaza samaki Liwatoni, Kaunti ya Mombasa ambapo ukarabati wa soko na kiwanda cha samaki unakumbwa na changamoto kufuatia madai ya ufisadi.

  • Tags

You can share this post!

Maraga, Mutunga wanguruma

TAHARIRI: Usomaji wa bajeti usiwe wa mzaha