• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:28 AM
Raia watatu wa kigeni watiwa mbaroni Ruiru kwa kupatikana na pesa bandia

Raia watatu wa kigeni watiwa mbaroni Ruiru kwa kupatikana na pesa bandia

Na LAWRENCE ONGARO

WASHUKIWA watatu wa kigeni kutoka nchini Cameroon, walinaswa na fedha bandia katika eneo la BTL mjini Ruiru mnamo Jumatatu jioni.

Afisa wa upelelezi katika kaunti ndogo ya Ruiru Bw Cyrus Ombati, alisema Francis Proper, 44, Job Kentong, 31, na Njikam Omar, 37, walipatikana wakiwa na fedha za kigeni za dola, pauni, na shilingi za Kenya, zote zikiwa na thamani ya Sh362 milioni.

Alieleza kuwa maafisa wa upelezi walipata habari kutoka kwa wakazi wa BTL kuwa kuna watu fulani waliokuwa wanajifungia ndani ya jumba fulani mchana kutwa bila kuonekana nje.

“Maafisa hao walipofika eneo hilo walipata fedha hizo na dhahabu ya kiwango cha kilo 320 huku uchunguzi wa uhalali wake ukianzishwa,” alisema Bw Ombati.

Afisa huyo alieleza kuwa maafisa hao walipata fedha hizi pamoja na mashine ya kutengenezea fedha hizo bandia.

Alizidi kueleza ya kwamba kwa muda wa wiki kadha wamekuwa wakifanya upelelezi kuwasaka washukiwa hao ambao inadaiwa wamekuwa wakijificha huku wakiendesha shughuli hizo haramu.

“Tunawapongeza wananchi kwa kutupatia habari kuhusu washukiwa hao. Tutaendelea kufanya juhudi kuona ya kwamba biashara haramu za aina hiyo haziendelei mhjini Ruiru na vitongoji vyake,” alisema Bw Ombati.

Alisema maafisa wa upelelezi wamewatia mbaroni washukiwa kadha ambao wamekuwa na shughuli za aina hiyo chini ya miaka miwili iliyopita.

Alizidi kueleza kuwa eneo hilo ni jumba moja ambalo linaendelea kujengwa ila halijakamilika kabisa.

Mnamo Februari 2019 katika eneo la Kwihota mjini Ruiru maafisa wa upelezi walinasa fedha bandia za thamani ya Sh32.6 milioni na kilo 70 za dhahabu bandia.

Bw Ombati alieleza kuwa washukiwa wanaendelea kuhojiwa ambapo baada ya hapo watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupatikana wakitengeneza fedha bandia na dhahabu.

  • Tags

You can share this post!

Msafara wa Suluhu wasababisha msongamano Mombasa Road

Rais Suluhu akagua gwaride la heshima la kijeshi