• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Rais Suluhu akagua gwaride la heshima la kijeshi

Rais Suluhu akagua gwaride la heshima la kijeshi

Na SAMMY WAWERU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa na kikosi cha kijeshi cha Kenya (KDF).

Hatua hiyo ni mila, utamaduni na itikadi za Kenya Rais wa kigeni anapowasili nchini, kama njia ya kuonyesha heshima.

Mama Samia alitua nchini Jumanne, kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), jijini Nairobi, dakika chache kabla ya saa nne asubuhi, ambapo alilakiwa na Waziri wa Masuala ya Kigeni Bi Raychelle Omamo, Balozi Amina Mohamed (Michezo) pamoja na Kaimu Gavana wa Nairobi Bi Anne Kananu.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku mbili Kenya, kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta.

Tayari, amefika katika Ikulu ya Rais, jijini Nairobi, na kulakiwa rasmi na Rais Kenyatta.

Mizinga 21 imefyatuliwa na kikosi cha kijeshi Kenya, kama ishara ya heshima kwa Rais huyo wa Tanzania.

Mama Samia pia amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa na maafisa wa KDF, Ikulu ya Rais Nairobi.

Ziara ya Rais Samia nchini inalenga kuimarisha uhusiano wa Kenya kibiashara na kidiplomasia, ili kuimarisha uchumi wa mataifa haya mawili.

Mama Samia alimrithi Dkt John Pombe Magufuli Machi 2021, kufuatia kifo cha Rais huyo wa awamu ya tano Tanzania.

  • Tags

You can share this post!

Raia watatu wa kigeni watiwa mbaroni Ruiru kwa kupatikana...

Ruto atengwa kwenye mapokezi ya Suluhu