• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Rais Kenyatta aalikwa awe mgeni wa heshima Tanzania itakapoadhimisha uhuru wa miaka 60

Rais Kenyatta aalikwa awe mgeni wa heshima Tanzania itakapoadhimisha uhuru wa miaka 60

Na SAMMY WAWERU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemwalika Rais wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta kuungana na nchi hiyo katika maadhimisho ya Sikukuu ya uhuru wa kujitawala ambapo Desemba taifa hilo litaadhimisha miaka 60.

Rais Suluhu ambaye Jumanne alianza ziara yake ya siku mbili Kenya, alitoa mwaliko huo Jumanne.

Tanzania huandaa hafla ya kifaifa Desemba 9, kila mwaka kama ukumbusho wa taifa hilo ambalo ni jirani ya Kenya, kupata uhuru wa kujitawala kutoka kwa serikali ya mkoloni.

“Ninatumia jukwaa hili kumualika kaka yangu Uhuru Kenyatta kama mgeni wa heshima Tanzania ikiadhimisha miaka 60 ya uhuru mwaka huu,” akasema Rais Suluhu katika hotuba ya pamoja katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi.

Rais Suluhu alisema tayari “nimeshazungumza na ndugu yake Rais Kenyatta na kumpa mwaliko rasmi.”

Katika kikao cha hotuba ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao, ilipepereshwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari, baada ya wawili hao kufanya mkutano wa faragha.

Walisema walijadiliana mengi kuimarisha uhusiano wa Kenya na Tanzania kibiashara, kiuchumi na pia kidiplomasia.

Uimarishaji wa miundomsingi ya usafiri na uchukuzi kwa njia ya barabara, hewa na majini, ni kati ya masuala yaliyojadiliwa, kwa mujibu wa maelezo ya Rais Kenyatta.

Mwaliko wa kumtaka Rais Kenyatta aungane na Tanzania Desemba 9, 2021, unatafsiriwa kama njia mojawapo kuonyesha utangamano wa mataifa haya mawili, na zaidi ya yote Rais Suluhu amerudisha mkono wa shukrani kwa serikali ya Kenya kutokana na mapokezi ya heshima na ya hadhi ya juu aliyopokea baada ya kutua nchini.

Wanajeshi wa Kenya (KDF) walifyatua mizinga 21, kuashiria heshima ya ziara ya Rais Suluhu nchini.

Rais huyo pia alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa na maafisa wa cheo cha juu katika jeshi la Kenya, katika Ikulu ya Rais Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Sergio Ramos roho juu kuongoza Real Madrid kuangusha...

Kutokuwepo kwa Mbappe si kisingizio cha PSG kupigwa na...