• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Ruto alionya bara kuhusu mapinduzi

Ruto alionya bara kuhusu mapinduzi

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto ameonya mataifa ya bara la Afrika dhidi ya kutumia mapinduzi kusuluhisha tofauti za kisiasa na badala yake kuzingatia michakato ya kidemokrasia.

Huku akiwahimiza viongozi wa nchi za Afrika kusikiza sauti za wananchi na kuheshimu maamuzi yao, alisema ni kupitia michakato ya kidemokrasia pekee ambapo raia wataweza kuwafanya viongozi kuwajibika.

Akizungumza Jumapili, Septemba 3, 2023 katika Kongamano la Vijana Afrika kuhusu Hali ya Mabadiliko ya Tabianchi 2023 lililoandaliwa katika ukumbi wa Kimataifa wa KICC, Dkt Ruto alisema kuzingatia michakato ya demokrasia kutawezesha mazingira bora kwa uchumi kustawi.

“Ni sharti turuhusu watu kufanya maamuzi. Chaguzi zinapaswa kumaanisha kitu. Ni sharti tukome kuvuruga chaguzi na demokrasia,” alisema Rais Ruto.

Dkt Ruto aliyeandamana na Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Akinwumi Adesina na Waziri wa Mazingira Soipan Tuya, alifichua kuhusu mipango ya kujumuisha mwakilishi wa vijana katika Muungano wa Afrika (AU).

Aliwahimiza vijana kuchukua nafasi yao katika mdahalo kuhusu mabadiliko ya tabianchi akisema kizazi hicho kina nguvu na sauti yao haiwezi kuendelea kupuuzwa.

“Tutahakikisha kuwa kongamano lijalo la AU lina vijana, si tu kama hadhira, bali wakiwa na nguvu kuhusu wanachofikiri muungano huu unapaswa kufanya,” alisema.

Kuhusu thamani ya raslimali barani Afrika zinazozuia uharibifu wa mazingira, Rais alisisitiza kuwa thamani hiyo ni sharti ihesabiwe ipasavyo.

Alitoa wito kuanzishwa kwa soko la raslimali hizo linaloambatana na viwango vya bei zilizoidhinishwa kimataifa.

“Hatutachukua malipo duni. Raslimali zetu za kuzuia uharibifu wa mazingira ni sharti ziwajibikie mali yetu na thamani yake kuhesabiwa ipasavyo.”

Aidha, alitoa wito kwa Afrika kutumia nafasi zilizopo katika sekta ya kilimo kuunda ajira na kupanua viwanda vya kuongezea bidhaa thamani.

Alihimiza mataifa makuu kuzingatia mikataba iliyowekwa kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Dkt Adesina alisema AfDB imejitolea kuimarisha uwezo wa bara hili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Waziri Soipan aliwahimiza vijana kuzingatia mawazo ya kiubunifu kuhusu teknolojia zisizoathiri mazingira.

Wakati uo huo, wandani wa Kinara wa Upinzani Raila Odinga wameonya kuwa Kenya huenda ikalazimika kugeukia mbinu zinazotumiwa na baadhi ya mataifa ya Afrika iwapo masuala yanayohusu chaguzi zilizoingiliwa hayatasuluhishwa kabisa.

Gavana wa Siaya, James Orengo, na Seneta Oburu Oginga walionya kuwa Wakenya huenda wakalazimika kutumia njia mbadala za kutekeleza haki zao kidemokrasia ikiwa watahisi sauti yao inapuuzwa na serikali.

Ingawa hawakutaja waziwazi hatua ambayo raia wangechukua, wanasiasa hao walisema Kenya ipo hatarini kutumbukia kwenye misukosuko ya kisiasa inayotikisa mataifa mengine ya bara la Afrika huku raia wakiashiria ghadhabu yao.

“Afrika inaashiria kuwa bara dhaifu mno. Udhaifu huu unatokana na michakato isiyo ya kidemokrasia. Ikiwa hatuwezi kuungana na kusuluhisha suala la kitaifa la chaguzi, watu watasaka mbinu mbadala,” alisema Orengo.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuondoa visa kwa Waafrika wanaozuru Kenya

Ajabu mume na mke wakubaliana kuchuuza uroda ili wapate mali

T L