• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Saint George Ethiopia, Wakenya watakia Matasi afueni baada ya ajali mbaya ya barabarani

Saint George Ethiopia, Wakenya watakia Matasi afueni baada ya ajali mbaya ya barabarani

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA wa soka nchini Ethiopia, Saint George FC wameungana na Wakenya kumtakia kipa Patrick Matasi na familia yake afueni ya haraka.

Matasi, 33, alihusika katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kapsabet akisafiri pamoja na familia yake wakielekea mjini Nairobi kutoka nyumbani katika Kaunti ya Kakamega mnamo Jumanne jioni.

Kupitia mtandao wake wa kijamii, Saint George, ambayo iliajiri Matasi kwa kandarasi ya miaka mitatu mnamo Oktoba 18, 2018, ilisema, “Tumpokea habari kuwa Patrick Matasi, ambaye ni kipa wa Saint George, amepata ajali akiwa na familia yake. Tunamtakia afueni ya haraka.”

Habari zinasema kuwa gari ndogo alimokuwa akisafiria kipa huyo wa zamani wa AFC Leopards, Posta Rangers na Tusker pamoja na mke wake na mtoto wao wa kiume, lilipoteza mwelekeo katika eneo la Lessos na kubingiria mara kadhaa.

Wasamaria wema walifika katika eneo la ajali na kuwasaidia kuwafikisha katika hospitali ya Kapsabet. Habari za mwanzo zinasema wote walijeruhiwa. Matasi, ambaye aliwahi kuwa kipa nambari moja wa Kenya, alilalamika kuwa na maumivu kifuani.

Taarifa hizo zinaongeza kuwa hawamo hatarini. Gari lao la aina ya Vitz liliharibika vibaya. Kandarasi ya Matasi na Saint George imeratibiwa kukamilika mwisho wa mwezi huu wa Juni. Klabu nchini Kenya na Tanzania zinasemekana zikoa tayari kutafuta huduma zake.

You can share this post!

Huzuni pacha wakifa baharini

Mbunge aitaka serikali ijenge shule zilizozama