• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Serikali yabuni njama kuunda maeneo mapya

Serikali yabuni njama kuunda maeneo mapya

Na GEORGE SAYAGIE.

SERIKALI imebuni njama mpya kuunda maeneobunge 70 zaidi kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani, siku chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kutaja mpango huo kuwa kinyume cha Katiba.

Taifa Leo imebaini kuwa kwenye mpango huo mpya, serikali tayari imeanza kupokea maoni kutoka kwa umma kuhusu mipaka, makao makuu na sehemu ambako maeneo hayo yatabuniwa.

Miongoni mwa kaunti zinazotarajiwa kufaidika kwa maeneobunge hayo ni Narok.

Ikiwa Wakenya watapitisha ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), kaunti za Kiambu, Nakuru na Kilifi ni miongoni mwa zile zitakazofaidika pakubwa, kwa kupata maeneobunge sita, matano na manne mtawalia.

Kaunti ya Nairobi imependekezwa kupata maeneobunge 12, hiyo ikiwa idadi kubwa zaidi.

Kaunti za Mombasa, Kwale, Machakos, Uasin Gishu, Narok, Kajiado na Bungoma zitapata maeneobunge matatu kila moja.

Kaunti za Meru, Trans-Nzoia, Bomet, Kakamega na Kisumu zitapata maeneobunge mawili zaidi kila moja huku Mandera, Embu, Makueni, Kirinyaga, Murang’a, Turkana, Pokot Magharibi, Nandi, Laikipia, Kericho, Siaya na Nyamira zikipata eneobunge moja kila moja.

Kulingana na mapendekezo ya BBI, Kaunti ya Narok imepangiwa kupata maeneobunge matatu zaidi, yakiwemo Narok Kaskazini, Narok Kusini na Trans Mara Magharibi.

Mnamo Ijumaa, mchakato wa kuigawa Kaunti Ndogo ya Narok Kaskazini uligeuka kuwa jukwaa la majibizano makali kuhusu mahali mipaka itakapowekwa. Ililazimu vikao hivyo kuahirishwa kwa wiki moja, baada ya wenyeji kutofautiana na serikali kuhusu utaratibu wa kuweka mipaka.

Kikao hicho kilihudhuriwa na mbunge Moitalel Ole Kenta (Narok Kaskazini), mwenyekiti wa Mamlaka ya Kulistawisha Eneo la Ewuaso Ngiro Kusini (ENSDA), Bw Seleina Ole Mwanik, mwanaharakati Maitamai Ololdapash, Bw Kelena Ole Nchoe kutoka Baraza la Wazee la Wamaasai (MCE), madiwani, machifu, manaibu wao na viongozi wa kijamii.

Idadi kubwa ya washiriki ilikubaliana na pendekezo la kukifanya kituo cha kibiashara cha Olokurto kuwa makao makuu lakini wakatofautiana na utaratibu kuhusu mipaka. Kikao hicho kilifanyika katika Shule ya Upili ya Kisiriri.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Narok, Bw Mutuku Mwenga, aliyekuwa akiongoza mkutano huo, alisema kaunti ndogo mpya itafika katika maeneo ya Oloropil, Enabelibel, Entiyani, Olokurto na Olpusimoru.

Hata hivyo, viongozi walipinga pendekezo hilo na kuomba muda zaidi kushauriana.

“Tunapinga kubuniwa kwa mipaka hii, kwani baadaye, kaunti ndogo mpya itafanywa kuwa eneobunge jipya. Ikiwa tutaafikiana na mpango huo, hilo litasababisha kubuniwa kwa eneobunge la Narok ya Kati, jambo ambalo tunalipinga kama wenyeji,” akasema Bw Nchoe.

Hata hivyo, Bw Mwenga alisema kuwa kugawanywa kwa kaunti ndogo hiyo katika maeneo mawili kunalingana na juhudi za serikali kupeleka huduma muhimu kama usalama kati ya zingine kwa wananchi.

Kwa sasa, kaunti hiyo ina kaunti ndogo sita, ambazo ni Narok Kaskazini, Kusini, Magharibi, Transmara Magharibi, Mashariki na Kusini, ambayo ilibuniwa kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

You can share this post!

Mjane wa Waititu apewa tiketi ya Jubilee Juja

Akasha: Shirika lahitaji miezi 6 kwa uchunguzi