• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Serikali yaendelea kuibua madai dhidi ya Harun Aydin

Serikali yaendelea kuibua madai dhidi ya Harun Aydin

Na SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Mating’i amepuuzilia mbali madai kuwa serikali ya Kenya imeomba msamaha Uturuki kwa kumfurusha mfanyabiashara raia wake, Harun Aydin, mwandani wa Naibu Rais, Dkt William Ruto.

Kwenye kikao na kamati ya usalama ya bunge jijini Mombasa, Ijumaa, waziri Matiang’i amesema ripoti za ujasusi zinaonyesha Bw Harun amekuwa akishiriki biashara alizotaja kuwa “haramu”.

Alisema serikali ilichukua hatua ya kumfurusha nchini, baada ya kufuatilia mienendo yake katika mataifa mbalimbali.

Dkt Matiang’i aliambia kamati hiyo kwamba raia huyo wa Uturuki hakufuata kikamilifu sheria za uhamiaji.

Waziri alieleza, idara ya usalama Kenya iliwasiliana na ile ya Uturuki katika mchakato mzima wa kumfurusha.

“Tuliwakabidhi Harun Aydin ili wajue hatua watakazomchukulia, sawa na tunavyofanya kwa raia wa Kenya nchi za kigeni wanapofanya makosa au kushiriki uhalifu,” Dkt Matiang’i akasema.

“Serikali ya Kenya haijaomba msamaha na hatutaomba msamaha kwa sababu hakuna kosa tulilofanya,” akasisitiza.

Hata hivyo, wakili wa Aydin, Bw Ahmednassir Abdullahi alichapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba serikali ya Uturuki haikuomba chochote kutoka kwa serikali ya Kenya kumhusu mteja wake.

“Inukuliwe: Serikali ya Uturuki haikutaka msaada wa aina yoyote kutoka kwa serikali ya Kenya kumhusu mteja wangu Bw Harun Aydin,” amesema wakili mkuu (SC) Ahmednassir.

Mapema Ijumaa, mwanablogu Dennis Itumbi alichapisha kwenye kurasa za mitandao, akidai kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Muysoka ametumwa na Rais Uhuru Kenyatta kuomba serikali ya Uturuki msamaha, kufuatia kufurushwa kwa Harun.

Kwenye maelezo ya Bw Itumbi, alisema kwamba “serikali imegundua Harun Aydin siye aliyelengwa kukamtwa” na kwamba “alikamatwa kimakosa”.

Waziri Matiang’i kwenye kikao na kamati ya bunge kuhusu usalama, amedai kwamba nambari za simu alizojaza Harun kwenye stakabadhi zake zilipopigwa zilipokelewa na watu wengine.

“Ikiwa nambari za simu alizojaza zinapokelewa na wanawake, hebu jiulize ni mtu wa aina gani?” akadadisi.

“Hakuwa na maelezo yoyote kumfuatilia,” waziri akaongeza, akitetea vikali hatua ya kumtimua.

Naibu Rais na wandani wake wanalalamikia kukamatwa na kufurushwa kwa raia huyo wa Uturuki kulichochewa kisiasa.

Wanasema alihangaishwa kwa sababu anahusishwa na Dkt Ruto.

You can share this post!

Kibarua cha Uhuru kupanga urithi OKA ikimkataa Raila

Karua aongoza Mlima kujipanga