• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 AM
Serikali yaweka mikakati ya kuwakabili wauzaji na watumiaji pombe haramu

Serikali yaweka mikakati ya kuwakabili wauzaji na watumiaji pombe haramu

Na LAWRENCE  ONGARO

BAADA ya wanawake wa kijiji cha Kimunyu kilichoko katika Kaunti ya Kiambu kuandamana wiki iliyopita kuhusu pombe haramu, serikali ilifanya kikao na washika dau kujadili mwelekeo mpya.

Mnamo Jumanne naibu kamishna, NACADA, na wakazi wa kijiji hicho walifanya kikao cha dharura huku maswala mengi yakiwemo pombe haramu na hali ya usalama yakijadiliwa.

Wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa maafisa tawala na polisi huku kila kitengo kikiwakilishwa.

Naibu Kamishna wa Gatundu Kusini Stanley Kamande aliyesimamia kikao hicho aliwahimiza wananchi kwa wakati wowote washirikiane vilivyo na wakuu wa usalama ili kukabiliana vilivyo na pombe hiyo haramu.

“Ninajua mkishirikiana vyema na maafisa wa usalama bila shaka tutafaulu kukabiliana na pombe haramu katika kijiji hiki,” alisema Kamande.

Alisema hata alitumwa na Kamishna wa Kaunti ya Kiambu Wilson Wanyanga akitoa mwito kwa wananchi wawe mstari wa mbele kuwapa maafisa wa usalama habari jinsi pombe hiyo inavyosafirishwa hadi Gatundu Kusini.

“Tunajua pombe haramu haipikwi hapo, lakini inasafirishwa hadi huko kutoka maeneo mengine,” alisema Bw Kamande.

Aliwataka wanaume wawajibike kwa familia zao kwa sababu pombe haramu imetajwa kuvunja ndoa nyingi kutokana na kukosa kutekeleza wajibu wao wa kifamilia.

Wiki iliyopita zaidi ya wanawake 100 waliandamana katika kijiji cha Kimunyu wakidai waume wao wamegeuka bwege huku wakishindwa kutekeleza tendo la ndoa.

Meneja mkuu wa NACADA katika eneo la Mlima Kenya Bw Amos Warui alisema kulingana na uchunguzi wao imethibitishwa kuwa maeneo mengi katika eneo hilo yamepunguza upikaji wa pombe na kuwahimiza wananchi wasilegeze kamba kushirikiana na polisi ili kukabiliana na hali hiyo.

“Ninataka mshirikiane na maafisa wa usalama ili kupambana na pombe hiyo haramu,” alisema Bw Warui.

Bi Teresia Wanjiru ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, alitaka serikali kuregesha baraza za machifu ili wananchi wawe na nafasi ya kutoka maoni yao.

“Tunaomba serikali irudishe vikao maarufu vya baraza ili machifu vijijini waimarishe utangamano miongoni mwa wanakijiji,” alisema Bi Wanjiru.

Alisema hakuna haja ya kuona wanaume wakivunja familia zao kwa sababu ya pombe, huku akiwataka wawajibike ipasavyo.

  • Tags

You can share this post!

WASONGA: Ruto, Raila wasaidie kutatua shida za Kenya si...

Kalonzo, Muthama, Mutua kupimana ubabe kampeni zikianza kwa...