• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Shirika la The Voice Kiambu lafadhili watoto mayatima

Shirika la The Voice Kiambu lafadhili watoto mayatima

Na LAWRENCE ONGARO

SHIRIKA la The Voice Kiambu County, limejitolea kuwafadhili watoto mayatima kwa lengo la kuwajali wasio nacho.

Mwenyekiti wa shirika hilo Bw Hamphrey Njenga, alisema shirika hilo lina wanachama wapatao 2,000 katika Kaunti ya Kiambu huku lengo kuu likiwa kuwahamasisha vijana ambao wangetaka kupata ujuzi katika kozi tofauti.

Mnamo Jumapili, shirika hilo likiandamana na wanachama wapatao 30 lilifanya ziara katika Dadas Community Centre mjini Thika na kuwapa bidhaa na vifaa vya thamani ya Sh50,000.

Walitoa chakula kama unga wa mahindi na unga wa chapati, mafuta ya kupikia, mchele, maharage, sabuni na nguo.

Bw Njenga alisema lengo lao kuu sio kupata faida yoyote lakini ni kujitolea kwa jamii hasa kwa wasiojiweza maishani.

“Tumekuwa tukizuru vituo vya watoto mayatima katika Kaunti ya Kiambu, huku tukiwapa vifaa muhimu kwa lengo la kuboresha hali yao ya maisha,” alisema Bw Njenga.

Alisema wanachama wote walio katika shirika hilo wana nidhamu ya hali ya juu kwa sababu kila mmoja hujitolea kuwasaidia wanufaika kwa chochote walicho nacho.

Alisema walipofika katika kituo hicho, walikuwa mstari wa mbele kuwapikia watoto hao chakula na kujumuika nao kwa lengo la kuwaleta pamoja na kuchangamsha.

Mkuu wa Dadas Community Centre, Bi Mary Wanjiru Kinyanjui alitoa pongezi kwa msaada waliopokea kutoka kwa shirika hilo akisema ni hatua nzuri na ya kuigwa na wengi.

“Sisi hapa katika kituo hiki tunao watoto mayatima wapatao 100 na wote wako kuanzia chekechea hadi Darasa la Tano,” alisema Bi Kinyanjui.

Alimpongeza mkurugenzi wa kituo hicho Bw Nitiri Harania, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba watoto hao wanaishi maisha mema.

“Hapa katika kituo hiki watoto hawa wanapokea malazi ya bure, chakula na mavazi huku watoto hao wakionyesha nidhamu ya hali ya juu kutokana na walimu wa hapa kuwapa mwongozo ufaao,” alisema Bi Kinyanjui.

Alisema baadhi ya watoto hao mayatima wanatoka katika makazi ya mabanda ya Thika kama Kiandutu, Kiganjo, na Athena.

Alitoa wito kwa wahisani wengine wenye nia njema wajitokeze ili kuendelea kuwasaidia watoto hao.

You can share this post!

Watambue wanawake bomba walio chini ya miaka 30

Mabadiliko ya makamanda wa polisi yafanyika Makadara