• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Siku ya Ukimwi Duniani: Vijana washauriwa wawe mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu Ukimwi

Siku ya Ukimwi Duniani: Vijana washauriwa wawe mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu Ukimwi

Na LAWRENCE ONGARO

VIJANA wameshauriwa kujiepusha na vitendo vya ngono kiholela ili waepuke Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa.

Vijana pia wamehimizwa kujiepusha na marafiki ambao wanaweza kuwapotosha katika maisha yao.

Waziri wa afya katika kaunti ya Kiambu, Dkt Joseph Murega, alisema vijana wanastahili kupewa mawaidha kuhusu Ukimwi kwa sababu wanapitia majaribio mengi maishani.

“Ninawahimiza wazazi pia wawe katika mstari wa mbele kuona ya kwamba wanawapa wana wao mawaidha kila mara wakiwa nyumbani,” alisema Dkt Murega.

Aliyasema hayo akiwa Juja leo Jumatano wakati wa kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.

Alitaja mambo matatu muhimu yanayostahili kuangamizwa kabisa katika jamii nayo ni uambukizaji wa virusi vya Ukimwi, mimba za mapema na dhuluma dhidi ya wanawake.

Alisema mara ya kwanza Ukimwi kutangazwa hapa nchini ilikuwa miaka ya themanini (80s) ambapo ni zaidi ya miaka 40 iliyopita.

“Mara ya mwanzo wakati maradhi hayo yalipotangazwa, yaliangamiza watu wengi kwa sababu hakukuwa na dawa kamili ya kudhibiti kama ilivyo leo hii,” alifafanua Dkt Murega.

Hata hivyo alieleza kuwa kwa sasa kuna dawa za kukabili makali ya Ukimwi kinyume na miaka ya nyuma.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na mashirika mengine tofauti kama vile Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini, World Vision, na Image Kenya.

Maafisa wake wakuu walihutubia wananchi na kuwahimiza vijana wawe makini na hali yao ya maisha.

Mwakilishi wadi (MCA) wa Murera Juja Bw John Walker Wokavi, alipongeza serikali ya Kaunti ya Kiambu kwa kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani.

Alisema hiyo ni njia moja ya kuonyesha jinsi kaunti hiyo ya Kiambu ilivyojitolea mhanga kuona ya kwamba inatangaza kwa wananchi umuhimu wa kujikinga wasiathirike na Ukimwi.

“Ninawahimizwa wazazi popote walipo wasikubali wana wao waangamie bure kwa kujiingiza katika vitendo vibaya na hatari vitakavyosababisha maambukizi ya Ukimwi,” alifafanua Bw Wokabi.

You can share this post!

Mwanamke ashukiwa kuwa gaidi

Juventus wajinyanyua ligini na kupepeta limbukeni...

T L