• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Mwanamke ashukiwa kuwa gaidi

Mwanamke ashukiwa kuwa gaidi

Na MARY WANGARI

WAPELELEZI kutoka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) mnamo Jumatano, Disemba 1, walimkamata na kumtia kizuizini mwanamke anayehusishwa na kundi la wapiganaji wa al-Shabaab.

Haya yamejiri huku serikali ikiimarisha mikakati ya kuhakikisha usalama kote nchini hasa maeneo ya pwani katika msimu huu wa sherehe.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 22, alikamatwa Jumanne jioni, Novemba 30, katika eneo la Tinderet, Kaunti ya Nandi.

Maafisa katika Kituo cha Polisi cha Sighor walifanikiwa kumfumania na kumkamata mshukiwa aliyekuwa akiishi na mwanamme katika kijiji cha Kamalambu, baada ya kudokezewa na wanakijiji waliomtilia shaka.

“Hofu ya wanakijiji ilithibitishwa wakati mwanamke huyo alipokuwa akihojiwa. Aliwaeleza makachero kwamba amekuwa nchini Somalia kwa miaka miwili huku akidai alikuwa ametekwa nyara na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Alshabab, mjini Kilifi, mnamo 2019,” ilisema taarifa kutoka kwa DCI.

Kulingana na DCI, mshukiwa alikiri kupokea mafunzo kuhusu ujuzi wa kutumia silaha, kushika watu mateka na matumizi mengineyo ya vilipuzi miongoni mwa maarifa mengine.

“Mwanamke huyo anasemekana kuhudhuria shughuli iliyokamilika hivi majuzi ya uteuzi wa makurutu wa KDF katika vituo mbalimbali,”

“Makachero wa Kitengo cha Kukabiliana na Ugaidi wameanzisha uchunguzi kuhusu suala hilo na wanaendelea kumhoji mshukiwa ili kupata habari zaidi,” ilisema DCI.

DCI ilipongeza wakazi wa Tinderet kwa kutoa habari hizo muhimu zilizowezesha kukamatwa kwa mshukiwa.

“Ushirikiano wa aina hii kati ya umma na maafisa wa polisi unahimizwa mno kwa sababu kudumisha usalama katika taifa ni jukumu letu kwa pamoja,” ilisema DCI.

Kisa hiki kinajiri wakati ambapo serikali imeimarisha usalama kote nchini na hasa katika maeneo ya pwani katika mwezi huu wa Disemba unaosheheni sherehe kadhaa.

  • Tags

You can share this post!

Mtambo unaochemsha na kuhifadhi maziwa yakisubiri kupata...

Siku ya Ukimwi Duniani: Vijana washauriwa wawe mstari wa...

T L