• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wabunge wataja ruzuku ya bei ya unga wakati wa Uhuru kuwa ni sakata

Wabunge wataja ruzuku ya bei ya unga wakati wa Uhuru kuwa ni sakata

NA CHARLES WASONGA 

WABUNGE Jumanne, walitaja mpango wa ruzuku ya unga wa mahindi ulioanzishwa na Rais Uhuru Kenyatta siku chache kabla ya kuondoka mamlakani kama sakata kubwa ambapo mabiliano ya pesa za umma zilifyonzwa.

Wabunge hao ambao ni wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo jana walidai kuwa mpango huo ulitumiwa kufadhili na kufanikisha kampeni za kisiasa za kuelekea uchaguzi wa Agosti 9, 2022 badala ya kuwakinga wananchi dhidi ya bei ya juu ya unga.

“Nadhani wasagaji unga walishirikiana na maafisa wa serikali kuiba pesa za umma kwa sababu unga huo wa Sh100 haukuwafikia wananchi. Hizi Sh2.5 bilioni ambazo kampuni 29 za kusaga unga zinadai hazikuwafaidi Wakenya bali watu fulani wachache na kampeni za kisiasa,” akasema Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Gathuka Kagombe (UDA).

Akaongeza: “Hamwezi kuthibitisha thamani ya pesa hizo kwa mwananchi. Vile vile, inaonekana kwamba hamjui ikiwa unga wa mahindi ulifikia watumiaji unga.”

Bw Kagombe alitoa malalamishi hayo Machi 14, 2023 wakati ambapo wawakilishi wa Muungano wa Kampuni za Wagaji Unga nchi (CMA) walifika mbele ya kamati hiyo kujibu maswali kuhusu mpango huo wa ruzuku ya unga wa mahindi.

Chini ya mpango huo ambao ulitekelezwa kwa kati ya Julai 19 hadi Agosti 19, serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilitangaza kwa unga ungeuzwa kwa Sh100 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Serikali ilichukua hatua hiyo kufuatia malalamishi ya umma baada ya bei ya unga kupanda hadi Sh230 kwa paketi moja ya kilo mbili. Hii, kulingana na wasagaji unga, ilichangiwa na uhaba wa mahindi nchini kutokana na mavuna duni na ukame ulioathiria mimea ya chakula mashambani.

Kwa upande wake, Mbunge wa Soy David Kiplagat alisema kuwa serikali iliyopita ya Bw Kenyatta alisababisha uhaba wa unga masokoni kimakusudi ili “kuanzisha mpango huo wa ruzuku kufaidi maafisa wake.”

“Awali, kabla ya mpango huo wa ruzuku kuanzishwa, unga ulikuwa ukipatikana madukani. Lakini unga huo ulipotea ghafla mpango huo wa ruzuku ulipoanzishwa kuanzia Julai 19, 2022. Wahudumu wa maduka ya supermarket walikuwa wakiwalazimisha wateja kununua bidhaa za thamani ya Sh1,000 ili waweze kupata paketi moja wa kilo mbili ya unga,” akasema Bw Kiplagat.

Lakini wawakilishi wa kampuni za kusaga unga walijitetea wakisea kuwa mpango huo wa ruzuku uliendeshwa kwa uwazi na wala haukutumiwa kufyonza pesa za umma.

Mohames Islam Ali, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kusaga unga ya Mombasa Millers Ltd alisema kuwa mpango huo ulikumbwa na uhaba wa mahindi ilhali hitaji lilikuwa kubwa.

“Kama wasagaji unga tulifanya kila tuwezalo kufikisha unga madukani. Lakini hitaji lilikuwa kubwa na mahindi yasiyo ya GMO hayakupatikana kwa urahisi ulimwenguni. Mahala ambapo tungepata mahindi hiyo ni Mexico lakini ingechukua muda wa zaidi ya mwezi mmoja kufikisha mahindi nchini. Kulikuwa na mahindi mengi Afrika Kusini lakini yalikuwa ya GMO ambayo yamepigwa marufuku nchini,” akaeleza Bw Islam.

Aliongeza kuwa ulikuwa msimu wa siasa na kampuni za usagaji unga zilikuwa katika presha ya kuwasilisha unga haraka.

Wakati wa kikao hicho kilichoongozwa na mwenyekiti wa Kamati hiyo John Mutunga, wanachama hao wa CMA waliwaambia wabunge kwamba walipa ushuru watalazimika kuwalipa Sh269 milioni kama iliyotokana na Sh2.5 milioni ambazo wanadai serikali.

“Kati ya Sh4.4 bilioni ambazo wanachama wetu walitumia kufanikisha mpango huo, serikali ilitulipa Sh1.7 bilioni pekee. Hii ina maana kuwa hatujalipwa jumla ya Sh2.5 bilioni kufikia sasa. Na pesa hizo zimezaa riba ya Sh269 milioni kwa miezi sita ambayo serikali imechelewesha kulipa pesa hizo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa CMA Paloma Fernandez.

Bi Fernandez alisema mkataba kati ya serikali na chama cha CMA ulisema kuwa serikali ingelipa wanachama wa muungano huo riba katika kiwango kinachotozwa na bei kwa sababu “pesa ambazo tulitumia kufadhili mpango huo wa ruzuku tulikopa kutoka kwa benki.”

Chama hicho kimewasilisha barua kadha kwa Waziri wa Fedha kikidai malipo ya Sh2.5 bilioni pamoja na riba lakini maombi yao hayajatekelezwa.

  • Tags

You can share this post!

Black Stars kukosa mazishi ya Christian Atsu

Haaland aweka rekodi mpya ya ufungaji mabao UEFA baada ya...

T L