• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Wabunge wataka CBC iondolewe, wasema ni ghali kwa wazazi na mzigo kwa walimu

Wabunge wataka CBC iondolewe, wasema ni ghali kwa wazazi na mzigo kwa walimu

Na BRIAN OJAMAA

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Bungoma, wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Elimu George Magoha, kuondoa mtaala wa elimu wa umilisi na utendaji (CBC ) au wauondoe kupitia bunge.

Wabunge hao Dan Wanyama (Webuye Magharibi) na Majimbo Kalasinga (Kabuchai), walisema kwamba nchi haiwezi kumudu mtaala huo mpya.

Walisema kwamba mtaala huo ni ghali mno kwa wazazi na ni mzigo kwa walimu.

“Kenya haikuwa imefikia kiwango cha elimu ya aina hiyo na kwa hivyo tunauliza rais na waziri kuondoa mtaala huo kabla hatujauondoa kupitia bunge,” alisema Bw Majimbo.

Bw Wanyama alionya kuwa iwapo mtaala huo wa CBC hautaondolewa, watoto kutoka familia masikini hawataweza kwenda shule.

“Kuna vitu vingi vinavyohitajika kununuliwa na wazazi kwa watoto wao kusoma na wazazi wengi hawawezi kumudu,” akasema.

Walidai kwamba rais anataka kuharibu mfumo wa elimu na wakashangaa kwa nini hakushauriana na wadau kabla ya kuanzisha mtaala huo.

“Tunataka serikali kurudia mfumo wa zamani wa elimu kwa kuwa huu ni wa kuharibu watoto wetu,” akasema.

Bw Kalasinga alisema hata walimu hawaelewi vyema mtaala huo.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yakataa kusitisha uchunguzi wa matamshi ya chuki

UDA yataka Matiang’i achunguze vurugu

T L