• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:07 PM
Wahasiriwa wa mkasa wa moto Mukuru-Kayaba wapokea msaada

Wahasiriwa wa mkasa wa moto Mukuru-Kayaba wapokea msaada

Na SAMMY KIMATU

FAMILIA zaidi ya 300 zilizopoteza makao yao baada ya moto kuteketeza nyumba zao katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, South B zimepata msaada.

Mwakilishi wa wadi ya Landi Mawe, Bw Herman Azangu Kaimosi aliwapatia unga wa mahindi, sukari na mchele.

Katika hotuba yake, Bw Azangu aliwaomba wakazi kuwakaribisha wawaniaji viti mbalimbali na kusikiliza sera zao na kuwasihi vijana wajiepushe na ghasia.

“Kila mwanasiasa ana haki ya kuja huku Mukuru ili kuuza sera zake. Hata hivyo, vijana ninawasihi msikubali kutumiwa na wanasiasa kuzua rabsha,” Bw Azangu akanena.

Moto huo ulitokea mwendo wa saa mbili za usiku siku tatu kabla ya mkesha wa Mwaka Mpya wakati ambapo wakazi wengi walikuwa wamesafiri kuelekea maeneo ya mashambani.

Mali ya thamani isiyojulikana iliteketea na kuwa majivu huku maafisa wa usalama wakianzisha uchunguzi wao ili kubaini kilichosababisha moto.

Chifu wa eneo hilo, Bw Paul Muoki Mulinge alihakikishia wakazi kwamba barabara zitatengwa ili kupisha njia za kutumiwa na magari wakati wa dharura.

Viongozi wa awali wamelaumiwa kwa sakata ya ardhi baada ya kudaiwa kuuzia mabwanyenye nafasi zilizokuwa za barabara hivyo kusababisha magari ya kuzima moto kukosa njia wakati wa kuja kuzima moto katika mitaa ya Mukuru.

  • Tags

You can share this post!

AS Monaco wamfuta kazi kocha Niko Kovac

West Ham wapaa baada ya kupepeta Palace ligini

T L