• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Wake wa Magavana nao wataka ofisi zao zitengewe mgao bajeti

Wake wa Magavana nao wataka ofisi zao zitengewe mgao bajeti

NA MARTIN MWAURA

MUUNGANO wa Wake wa Magavana Nchini unataka watengewe mgao wa fedha ili kufadhili miradi ambayo wanazamia katika kaunti zao.

Bi Emily Nyaribo, mkewe Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo alisema wanastahili mgao huo kwa sababu wao hushirikiana na waume wao kufanikisha miradi mbalimbali.

Alisema mara nyingi wao hukumbana na visa vingi ambapo wao huhitajika kutoa msaada ilhali hawana mgao wao wala nafasi yao haithaminiwi na serikali.

Kwa hivyo, Bi Nyaribo aliyataka mabunge ya kaunti yapitishe sheria za kutengea bajeti afisi za wake wa magavana kurahisisha kazi yao ya kufanikisha miradi kwa raia. Alikuwa akizungumza katika Hospitali ya Level Four ya Kirwara mnamo Alhamisi.

Bi Nyaribo alikuwa amehudhria hafla ya kuzindua uhamasisho dhidi ya ugonjwa usonji (Autism) hospitalini humo ambapo aliandamana na Mkewe Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata, Bi Mary Wambui na mkewe Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Pia wake wa magavana wa Nyeri, Migori na Kiambu walikuwepo pamoja na wake wa wabunge wa sasa na wa zamani. Wakati wa hafla hiyo, wake wa magavana pia walitaka nafasi yao itambuliwe rasmi na serikali.

“Hatuna bajeti na tunalazimika kutegemea hisani ya waume wetu kuhusu miradi tunayoifanya,” akasema Bi Nyaribo.

“Tungependa kuwaomba madiwani na magavana waharakishe mchakato wa kutambua afisi za wake wa magavana ili tuwe na bajeti na kuunga kazi ambayo tunafanya,” akaongeza.

Bi Agnes Ochillo, Mkewe Gavana wa Migori Ochillo Ayacko alisema wao wanasukumwa na wito na nia ya kusaidia ndiposa wanashiriki miradi ambayo inasaidia wananchi kupitia afisi za magavana.

“Tulisafiri nao wakati ambapo walikuwa wakifanya kampeni na tukatoa ahadi nao kwa raia. Wakati huu ambapo wameshapata viti ni vyema iwapo tutawasaidia waume wetu kutimiza ahadi zao,” akasema Bi Ochillo.

“Huwa hatupokei mishahara na huwa tunayaacha majukumu yetu ya kila siku ili kushiriki miradi ya kuinua jamii kama ile ya afya. Tunajitafutia pesa za kufadhili miradi hiyo jambo ambalo si rahisi,” akaongeza Bi Ochilo ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Muungano wa Wake wa Magavana Nchini.



  • Tags

You can share this post!

Ukabila ulivyokolea katika Serikali Kuu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tutumie vizuri Kumi hili la Mwisho la...

T L