• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wanahisa Embakasi Ranching waitaka serikali iharamishe hatimiliki 25, 000 zilizotolewa na Uhuru Kenyatta 

Wanahisa Embakasi Ranching waitaka serikali iharamishe hatimiliki 25, 000 zilizotolewa na Uhuru Kenyatta 

NA MWANGI MUIRURI
WANAHISA wa Kampuni ya Embakasi Ranching sasa wanataka hatimiliki 25,000 ambazo serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta iliwapa mwaka wa 2022 ziharamishwe.

Badala yake, wanaitaka serikali ya sasa ya Rais William Ruto izindue harakati hizo upya baada ya kupiga msasa wanahisa halisi.

Mwenyekiti wa bodi ya usimamizi katika kampuni hiyo Bw John Njoroge alisema kwamba serikali ya Bw Kenyatta ililenga kutoa hatimiliki 50, 000 katika mashamba hayo ya ekari 16, 000.

“Ajabu ni kwamba, wanahisa wetu ni takriban 3, 000 na kwa pamoja kuna ploti 30, 000. Kati ya hatimiliki hizo 25, 000 zilitolewa, kumezuka malalamishi 19, 000 ambapo mashamba ya wengine yamekabidhiwa watu ambao sio wetu,” akasema.

Aidha, Bw Njoroge alisema kwamba hatimiliki hizo zilitolewa kinyume na sheria kwa kuwa kuna ilani ya mahakama ya 2012 ambayo ilizima ugavi na uhalalishaji wa umiliki katika mashamba ya Embakasi.

Ilani hiyo ambayo Taifa Leo Dijitali imeona, ilitokana na kesi nambari 395 ya 2011 ambapo Bi Josephine Njeri Gakami aliomba mahakama izime harakati hizo mbili kwa hofu kwamba orodha ya wanahisa ilikuwa imevurugwa na kupenyeza wakora wa unyakuzi.

Mnamo Februari 15, 2012, Jaji Philemona Mwilu alitoa uamuzi kwamba harakati hizo zizimwe hadi kesi ya kuthibitisha ukora huo uliodaiwa isikizwe na kuamuliwa.

Bw Njoroge aliongeza kuwa serikali ya Bw Kenyatta ilipuuza kesi na amri ya Jaji Mwilu kwa kuwa hadi sasa haijaamuliwa, hivyo basi kugeuza hatimiliki hizo 25, 000 kuwa ukaidi wa mahakama.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuondoa masoko yaliyoko kandokando mwa barabara...

Rais Ruto – Wakenya watakaopanda miti kutuzwa na...

T L