• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Washukiwa 11 wa kundi la MRC waliokamatwa wachunguzwa

Washukiwa 11 wa kundi la MRC waliokamatwa wachunguzwa

Na MOHAMED AHMED

POLISI katika kaunti ya Mombasa wanachunguza nia ya watu 11 waliokamatwa Ijumaa alasiri kwa kushukiwa kuwa wanachama wa Kundi la Mombasa Republican Council (MRC).

Washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Mwaweni Likoni na polisi wanasema walikuwa na umri wa kati ya miaka 34 na 64.

Kwa mujibu wa polisi, washukiwa hao walifumaniwa wakiwa kwenye mkutano haramu na sare na vitambulisho vya kundi la MRC pamoja na bendera ya kundi hilo.

Mkuu wa DCI Richard Koywer alisema washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Port Kisiwani Mombasa huku uchunguzi ukiendelea.

Alisema kwamba walikiuka kanuni za kuzuia msambao wa virusi vya corona.“Watasalia katika seli za polisi hadi Jumatatu ambapo watafikishwa mahakamani kwa kuandaa mkutano haramu na kukosa kuzingatia masharti yaliyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona,” akasema Koywer.

Afisa huyo alisema kwamba vitambulisho vingi na stakabadhi zilizoonyeshwa kuwa washukiwa hao 11 walikuwa wanachama wa MRC vilipatikana msituni mtaani Likoni.

Hata hivyo, Msemaji wa MRC Randu Nzai alikanusha madai kwamba washukiwa hao walikuwa wakipokea mafunzo ya kusajiliwa katika kundi hilo.

MRC ni kundi ambalo limekuwa likipigania uhuru wa ukanda wa Pwani ili ujitenge na maeneo mengine ya Kenya.Kundi hilo pia lilikanusha madai ya serikali kwamba lina uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Shabaab linalopigana katika nchi jirani ya Somalia.

Wizara ya usalama wa ndani imekuwa ikihusisha visa vya uhalifu eneo la Pwani na kundi hilo.Mnamo Disemba 2020, polisi katika eneobunge la Jomvu waliwakamata watu zaidi ya 100 wanaohusisha na MRC huku 90 kati yao wakiwa wanawake.

Washukiwa hao walikuwa wakikula kiapo ili kujiunga na MRC.Kwa sasa mikutano ya hadhara imepigwa marufuku kote nchini kama njia mojawapo ya kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona.

Kulingana na polisi, washukiwa hawakuwa na kibali cha kuandaa mkutano wa hadhara na wanaendelea kuchunguza nia yao kukiuka kanuni za serikali kwa kukutana.Kundi hilo limekuwa likikanusha madai ya serikali kwamba linahusika na vitendo vya uhalifu.

You can share this post!

DINI: Hata kama hatumwoni, Bwana Mchungaji Mwema huwa nasi...

Serikali ya TZ sasa yaweka mitambo ya oksijeni hospitalini