• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Watabiri hewa Pwani wachanganya wakazi

Watabiri hewa Pwani wachanganya wakazi

Na SIAGO CECE

HOFU kuhusu ukame imekumba ukanda wa Pwani baada ya wataalamu wa hali ya hewa kushindwa kubaini mvua itaanza kunyesha lini katika sehemu hiyo.

Akizungumza na Taifa Leo, mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa Kaunti ya Mombasa, Bw Charles Mwangi alisema kuwa mawimbi katika Bahari Hindi ndiyo yameathiri jinsi mvua inavyonyesha Mombasa.

Ingawa msimu wa mvua unafaa kuisha mwezi huu, Kaunti za Kwale, Kilifi, Mombasa, Lamu na Tana River zimepokea mvua kidogo.

Kwa mfano, mji wa Mombasa, umepokea asilimia 10 pekee ya mvua iliyotarajiwa tangu mwaka huu 2021 ulipoanza. Mvua hii inanyesha tu kwa dakika chache kabla ya jua na joto kurejea.

Hali hii imewatia wasiwasi wakulima wanaotegemea mvua, huku wengi wakihofia kuwa kutakuwa na ukame na uhaba wa chakula katika miezi ijayo.

“Hatuwezi kusema kuwa kiangazi kitaendelea na pia siwezi kuhakikisha kuwa msimu wa mvua umeisha. Ninachoweza kusema ni kuwa, mvua itachelewa na kunyesha baada ya msimu uliotabiriwa. Hii imewahi kufanyika awali,” Bw Mwangi alisema.

Mawimbi hayo pia yamefanya sehemu nyingine za nchi kama vile maeneo ya kati na magharibi kupokea mvua zaidi kuliko kawaida.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na ufugaji ya Kenya (KALRO) Finyange Pole, serikali za kaunti za Pwani zinapaswa kutenga pesa ili kufanya miradi ya kuteka maji ya mvua yatakayotumiwa na wakulima kunyunyizia mimea hasa wakati wa kiangazi.

Alisema kwamba mvua inaponyesha katika sehemu nyingine nchini, maji yote huteremka na kuenda katika Bahari ya Bara Hindi.

“Wakati huu, hatuwezi kamwe kutegemea mvua kwa mimea yetu kwa sababu hali imebadilika. Unaweza kupanda mimea ukifikiri mvua itanyesha kisha ikose,” Bw Pole alisema.

Pia, aliwahimiza wakulima kupanda mimea ambayo haichukui muda mrefu kukomaa kama vile viazi vitamu na dengu, na pia kuchanganya mimea ya aina tofauti.

Wakati huu, wakulima wengi katika sehemu nyingine nchini wamefurahia kupoke a mvua zaidi kwa ajili ya mimea yao.

You can share this post!

Vigogo wa Pwani lawamani kwa maneno matupu

Matumaini ya mwafaka kati ya Israeli na Palestina yafifia