• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wazee kuuliza ‘miungu’ kabla ya kuamua sehemu ya kutakasa msitu wa Shakahola

Wazee kuuliza ‘miungu’ kabla ya kuamua sehemu ya kutakasa msitu wa Shakahola

NA MAUREEN ONGALA

WAZEE wa Kaya za Mijikenda, watategemea mwongozo wa miungu kuamua sehemu halisi ambapo matambiko yatafanywa kutakasa msitu wa Shakahola ambapo zaidi ya vifo 400 vya dhehebu linalohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie viligunduliwa.

Kutokana na pendekezo la kamati ya muda ya seneti iliyochunguza vifo hivyo kwamba serikali ya kaunti ya Kilifi inafaa kuwawezesha wazee kutekeleza matambiko yao, wazee wa Kaya ya Kilifi wamesema wako tayari punde tu watakapopewa idhini.

Kulingana na mratibu wa Chama cha Wazee wa Kaya za Mijikenda, Bw Tsuma Nzai, tambiko hilo litahusisha makundi matatu ya wazee wa Kaya kutoka kabila kubwa la Wagiriama.

Akiongea na Taifa Leo, Bw Nzai alisema eneo halisi la matambiko hayo litaamuliwa na miungu.

“Kwa kuwa ni ardhi ya Giriama iliyonajisiwa, matambiko hayo yatajumuisha wazee wa Kaya kutoka Weruni, Galana, na kaya za Godoma,” akasema.
Bw Nzai alisema kwanza, kikundi cha wazee kitachunguza msitu huo na kuamua mahali pa kufanyia matambiko hayo maalum kwa mwongozo kutoka kwa miungu.

“Wazee wataenda katika pembe zote za msitu na watakaa tu mahali watakapoelekezwa na miungu. Wataweka chungu chenye mchanganyiko wa mitishamba na hapo ndipo tutakapoanza rasmi matambiko,” alisema.

Baadhi ya vitu vinavyohitajika ni pamoja na fahali mwekundu mwenye kichwa cheupe, kondoo mweupe, mbuzi mwekundu na kuku mweusi, mweupe na mwekundu. Aidha, fahali mweusi na mbuzi mweupe pia watachinjwa.

“Tunamtumia ng’ombe mwekundu mwenye kichwa cheupe kwa kuwa ni ibada ya utakaso na ingetumika kutoa dhabihu na kutuliza miungu inayoambatana na kuombea amani,” alieleza.

Pia, kutakuwa na ngoma maalum ya kiganga na nyingine inayotambuliwa kama ngoma ya pini.

Ngoma hizo mbili daima huwekwa wakati wazee wanataka kubaini chanzo cha matukio ya kichawi na wakati wa kufurusha mapepo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee wa Mijikenda wa Kaya, Mzee Mwalimu Mwinyi, alisema matambiko hayo maalum huwa yanafanyika siku ya Alhamisi au Jumapili pekee.

Alieleza kuwa, wanaume na wanawake wakiwa wamevaa mavazi ya kitamaduni ya Mijikenda watafanya matambiko tofauti kwa siku tofauti.

“Taratibu hizi za utakaso ni maalum kwa jamii ya Mijikenda kwa kuwa zinalenga kufurahisha miungu na lazima zifanywe ipasavyo ili kuepusha matukio mengine kama hayo,” alisema.

Kulingana na ripoti ya kamati ya seneti iliyoongozwa na seneta wa Tana River, Bw Danson Mungatana, kamati ya bunge la kaunti ya Kilifi ilikuwa imefahamisha maseneta kuwa, wazee wa Kaya walikuwa wamepanga kukusanyika Shakahola kufanya maombi ya kimila na kutakasa eneo hilo.

“Changamoto ambayo wazee wa Kaya walikumbana nayo ilikuwa kwamba utakaso unahitajika kufanywa ndani ya msitu ambao hawawezi kuufikia kutokana na kuwa ni eneo lililozuiliwa kuingiliwa na watu ambao hawajaidhinishwa na serikali,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kamati hiyo ilishauri kuwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi iwasaidie Wazee wa Kaya kufanya utakasaji huo.

  • Tags

You can share this post!

Kenya ina bahati kunichagua rais kuwaongoza wakati huu...

Anne Amadi aanza kujitayarisha kung’atuka kama Msajili...

T L