• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wazee wa Nyumba 10 wadai mshahara

Wazee wa Nyumba 10 wadai mshahara

WAZEE 5,000 wa Nyumba Kumi katika Kaunti ya Kitui sasa wanataka serikali iwape mshahara kwa “kazi ngumu” wanayoifanya.

Wakizungumza Ijumaa baada ya mkutano katika Shule ya Msingi ya Central Kitui, walilalama kuwa serikali imepuuza mchango wao katika utawala.

Walisema kuwa wamekuwa wakihusika pakubwa kutatua mizozo, kuhamasisha wakazi pamoja na kukabiliana na visa vya uhalifu kwenye maeneo yao.

Bi Elizabeth Gichee ambaye ni mmoja wa viongozi hao kutoka Mjini Kitui alisema kazi yao ni ngumu kutokana na changamoto tele wanazokabiliana nazo.

“Simu yangu hupigwa mara kwa mara hata usiku. Nami husitisha shughuli na kukimbia katika eneo la tukio,” alieleza.

Aliongeza kuwa wazee hao wa Nyumba Kumi wamekuwa wakitumia hela zao nyingi kusafiri hadi maeneo mbalimbali kunakoripotiwa tukio.

“Ninatumia hela nyingi kuwasiliana na machifu, manaibu chifu pamoja na waathiriwa. Mimi ni mwuzaji mdogo wa kuku na sehemu ya mapato yangu ya kibiashara yanaishia katika shughuli zinazohusiana na kazi hii ya Nyumba Kumi,” akasema.

Mohammed Abdallah ambaye ni mzee mwingine wa Nyumba Kumi eneo la Kitui Mjini, alisema mswada uliowasilishwa Bungeni kupendekeza wazee wa kamati hizo maalum za kijamii za usalama walipwe mishahara, umejikokota sana na sasa wamepoteza matumaini.

“Hatuhitaji mishahara minono bali malipo kidogo tu ya kututia motisha tunapohudumia jamii,” alihoji Bw Solomon Kimanzi, mwenyekiti wa wazee wa Nyumba Kumi katika Kaunti ya Kitui.

Kaunti ya Kitui ina jumla ya wazee 5,934 wa Nyumba Kumi ambao wamekuwa wakishirikiana na machifu na manaibu wa chifu kuhudumia wakazi.

Wazee hao hufanya kazi kwa kujitolea na huteuliwa moja kwa moja na machifu kutoka miongoni mwa wakazi eneo fulani.

Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ushirikishi ya 2013, unalenga kuhakikisha kuwa wazee wa Nyumba Kumi wanalipwa rasmi mshahara.

Mswada huo pia unapiga marufuku wazee kuteuliwa na machifu, na badala yake unapendekeza waajiriwe na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Umma (PSC).

Kwa sasa, wazee hao wa vijiji wanategemea fedha kidogo wanazopewa kwa hiari na makamishna wa kaunti pamoja na mashirika yasiyo ya serikali.

You can share this post!

Sherehe za Mashujaa marufuku kaunti 46

Viongozi wa Gusii mbioni kuunda chama chao cha siasa