• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Sherehe za Mashujaa marufuku kaunti 46

Sherehe za Mashujaa marufuku kaunti 46

Na GEORGE MUNENE

SERIKALI imepiga marufuku sherehe za Mashujaa katika kaunti zote 46 katika juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Sherehe ya kitaifa itakayoandaliwa katika Kaunti ya Kirinyaga na kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, itaendelea kama ilivyopangwa.

Katibu katika Wizara ya Masuala ya Ndani, Dkt Karanja Kibicho, Ijumaa aliwataka Wakenya kufuatilia sherehe za kitaifa zitakazofanyika katika uwanja wa Wang’aru kupitia runinga zao.

“Sherehe za Mashujaa hazitafanyika katika kaunti nyingine 46 ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona,” akasema.

Katibu huyo alisisitiza kwamba serikali inataka kulinda maisha ya Wakenya, akieleza kuwa hiyo ndiyo sababu ya kufutiliwa mbali kwa sherehe hizo katika kaunti nyingine kote nchini.

Makamishna wa kaunti waliagizwa kuhakikisha kuwa agizo hilo limezingatiwa.

Akihutubu Ijumaa katika eneobunge la Mwea, alipokagua ujenzi wa uwanja huo, Dkt Kibicho alisema serikali inachukua kila hatua kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Uwanja huo unaojengwa kwa gharama ya Sh300 milioni, unatarajiwa kumalizika Oktoba 5.

Hata hivyo, ni watu 2,000 pekee ambao wataruhusiwa kushiriki kwenye hafla hiyo.

“Wakazi wengi walikuwa na matarajio makubwa ya kuhudhuria hafla hiyo ambayo itaongozwa na Rais Kenyatta. Hata hivyo, hilo halitawezekana kutokana na haja ya kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo,” akasema.

Alieleza kuwa kuna miradi mikubwa inayoendelea kujengwa katika eneo hilo, ambapo lazima ikamilishwe kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

“Kuna barabara zinazojengwa na mataa yanayowekwa katika miji mikubwa kote katika eneo hili. Kuna Ikulu Ndogo ya Rais inayojengwa huku uwanja mdogo wa ndege wa Wang’uru ukiendelea kufanyiwa ukarabati. Hiyo ni baadhi tu ya miradi inayoendelea ambapo lazima ujenzi wake ukamilike katika muda uliowekwa,” akasema.

You can share this post!

Korti yaamua Obure ana kesi ya kujibu sakata ya Sh1.3b

Wazee wa Nyumba 10 wadai mshahara