• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Waziri Keter alishwa faini ya Sh500,000 kwa kufeli kufika mbele ya kamati ya seneti kuhusu kawi

Waziri Keter alishwa faini ya Sh500,000 kwa kufeli kufika mbele ya kamati ya seneti kuhusu kawi

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Seneti kuhusu Kawi imemtoza faini ya Sh500,000 Waziri wa Kawi Charles Keter kwa kufeli kufika mbele yake Alhamisi kutoa maelezo kuhusu bei ya stima nchini.

Bw Keter aliamriwa kufika mbele ya kamati hiyo, inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina, kuelezea kile wizara inafanya kupunguza bei ya kawi hiyo kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.

Waziri huyo alikuwa amealikwa mnamo Septemba 3, 2021 lakini akafeli kufika ndipo kamati hiyo ikatoa amri (summons) kwamba afike Alhamisi, Septemba 23, 2021.

“Kamati hii imeghadhabishwa sana na kutofika kwake na hatuwezi kuvumilia mwenendo kama huu kutoka kwa mawaziri wa serikali. Kwa hivyo, kulingana na kanuni za bunge hili, tunamtoza faini ya Sh500,000 kwa kosa hilo,” akasema Mhandisi Maina aliyeonekana mwenye hasira.

Kulingana na sheria hiyo kuhusu Hadhi na Mamlaka ya Maseneta, afisa wa serikali aliyetozwa faini kama hiyo sharti atumie pesa zake binafsi kulipa na wala sio pesa za asasi anayosimamia.

Bw Maina alitoa adhabu hiyo kwa Bw Keter licha ya waziri huyo kutuma barua ya kuomba radhi kwa kamati hiyo akisema amesafiri ng’ambo kwa mkutano wa Shirika la Kimataifa la Atomiki unaoendelea nchini Austria.

Barua yake iliwasilishwa kwa Kamati hiyo na Katibu katika Wizara ya Kawi Joseph Njoroge. Katibu huyo alikuwa ameandamana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Usambazaji Stima Nchini, Kenya Power.

Kwa upande wake Seneta wa Narok Ledama OleKina alimshutumu waziri Keter kwa kile alichotaja kama kutelekeza wajibu wake.

“Huyo ni mkimbizi wa uwajibikaji ambaye anafaa kutozwa faini na alipe yeye binafsi. Hizo pesa zisitoke kwa wizara. Kwa kuwa amekuwa seneta anafahamu kanuni za bunge lakini ameamua kuzidharua,” akasema OleKina.

Maseneta wengine walioelekeza kero zao kwa Bw Keter, ambaye zamani alihudumu kama Seneta wa Kericho, ni; John Kinyua (Laikipia) na Prof Malachy Ekai (Turkana).

Afisa mwingine ambaye amewahi kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kukaidi amri ya kutakiwa kufika mbele ya kamati ya seneti ni Gavana wa Kitui Charity Ngilu.

Alipewa adhabu hiyo na Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC) mwaka 2020, wakati huo ikiwa chini ya uenyekiti wa Seneta wa Kisii Prof Sam Ongeri.

Adhabu hii dhidi ya waziri Keter inajiri siku moja baada ya kikao cha bunge lote la seneti kupitisha hoja ya ghadhabu (censure motion) dhidi yake na mwenzake wa Mafuta na Madini John Munyes.

Wawili hao walifeli kufika mbele ya maseneta Jumanne kuelezea kiini cha kupanda kwa bei ya mafuta kwa kiwango cha juu kupita kiasi sawa na kupanda kwa bei ya stima.

Hoja hiyo iliwasilishwa na kiongozi wa wachache James Orengo ambaye ni Seneta wa Siaya.

You can share this post!

Wakazi wafurahia hatua ya Rais Kenyatta kupandisha hadhi...

‘Wakenya 103 wamefia Uarabuni tangu 2019’