• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:11 PM
Wezi wa mifugo wauawa Samburu

Wezi wa mifugo wauawa Samburu

Na GEOFFREY ONDIEKI

 

Watu wawili wameuawa kwenye shambulizi kali la wizi wa mifugo eneo la Marti katika kaunti ya Samburu na kutoweka na mifugo takribani 521.

 

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, majambazi hao ambao wanakisiwa kutoka jamii hasimu eneo hilo walitoweka na mifugo baada kitendo hicho cha unyama.Shambulizi hilo linajiri siku tatu pekee baada ya wezi hao kuvamia kijiji hicho na kuiba mbuzi zaidi ya mia mbili.

 

Hata hivyo, polisi wanasema kuwa wanawasaka wezi hao hata ingawa hakuna mifugo yeyote iliyookolewa hadi sasa.Kamishna wa kaunti ya Samburu Bw Abdirazak Jaldesa alithibitisha watu kuuawa baada ya kupata majeraha mabaya ya risasi huku mmoja wao akiendelea kupokea matibabu katika hosipitali ya rufaa ya Samburu.

 

Bw Jaldesa alisema kuwa maafisa wa polisi wanaendelea kufanya msako ili kurudisha utulivu eneo hilo ambalo limekumbwa na visa vya wizi wa kila mara wa mifugo.

“Tunaendelea na juhudi za kurudisha mifugo iliyoibwa na kurejesha utulivu. Hatutachoka mpaka tuhakikishe tumewakamata washukiwa,” Jaldesa alisema.

 

Mtawala huyo alihimiza wakazi kutolipiza kisasi na badala yake kuwapa maafisa wa usalama muda wa kuwaandama wahalifu hao.Gavana wa kaunti hiyo Moses Lenolkulal aliomba serikali kutafuta suluhu ya kudumu na kumaliza tatizo la wizi wa mifugo ambalo limejiri kwa muda mrefu sasa.

 

Gavana huyo alikiri kwamba watu wengi wamepoteza maisha yao na wengine kuhama kufutia mzururu wa utovu wa usalama.”Tunahutaji suluhu ya kudumu kwa sababu watu wengi wasiokuwa na hatia wamefariki na mali kupotea. Nahimiza idara ya usalama wa kitaifa kuingilia kati na kumaliza utovu wa usalama eneo hili,” alisema.

 

Mbunge wa Samburu Kaskazini Bw Alois Lentoimaga alinyoshea idara ya usalama kidole cha lawama kwa kushindwa kukabili wezi wa mifugo. Aliomba waziri wa usalama wa ndani Bw Fred Matiangi kumaliza tatizo la wizi wa mifugo Samburu.

 

“Tunalaumu maafisa wa usalama kwa sababu shambulizi lilitekelezwa mita chache kutoka kituo cha polisi,” Bw Lentoimaga alisema.Miili ya waliofariki inaendelea kuhifashiwa katika hifadhi ya maiti ya hosipitali ya rufaa ya Samburu.

 

  • Tags

You can share this post!

CF Montreal anayochezea Wanyama yang’ata Cincinnati...

Al Ahly wakomoa Kaizer Cheifs na kutwaa taji la CAF...