• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Al Ahly wakomoa Kaizer Cheifs na kutwaa taji la CAF Champions League kwa mara ya 10 katika historia

Al Ahly wakomoa Kaizer Cheifs na kutwaa taji la CAF Champions League kwa mara ya 10 katika historia

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka kutoka Misri, Al Ahly, walijizolea kima cha Sh272 milioni baada ya kupepeta Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika uga wa Mohamed VI jijini Casablanca, Morocco na kunyanyua taji la Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League).

Mbali na kupokezwa tuzo hiyo, Al Ahly walioweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza kuwahi kutawazwa wafalme wa Klabu Bingwa mara 10, pia walifuzu kwa kipute cha kuwania Kombe la Klabu Bingwa Duniani.

Fowadi Mohamed Sherif alifunga bao na kuchangia jingine kwa upande wa Ahly waliowateremkia wapinzani wao baada Happy Mashiane wa Chiefs kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Magoli mengine ya Al Ahly yalifumwa wavuni kupitia Mohamed ‘Afsha’ Magdy na Amr El Solia.

Mataji 10 ambayo sasa yanajivuniwa na Al Ahly kwenye Klabu Bingwa Afrika yanaweka kikosi kingine chochote katika hali ngumu ya kufikia rekodi yao. Zamalek SC kutoka Misri na TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio wanaowafuata Al Ahly kwa karibu japo kila mmoja wao ametwaa ubingwa wa CAF Champions League mara tano pekee.

Kombe la Jumamosi lilikuwa la tatu kwa kocha Pitso Mosimane wa Al Ahly kunyanyua baada ya kuongoza waajiri wake kupepeta Zamalek SC 2-1 mnamo 2020 na kutwaa ubingwa wa CAF Champions League kwa mara nyingine. Aliwahi pia kuongoza Al Ahly kupepeta Mamelodi Sundowns kwenye fainali ya 2016.

Mosimane kwa sasa ndiye kocha wa pili kuwahi kutwalia Al Ahly taji la CAF Champions League mara mbili mfululizo baada ya Manuel Jose kufanikiwa kufanya hivyo mnamo 2005 na 2006.

Al Ahly walijibwaga ugani dhidi ya Chiefs wakipigiwa upatu wa kuibuka mabingwa ikizingatiwa kwamba ilikuwa mara yao ya 14 kunogesha fainali ya CAF Champions League.Aidha, motisha yao ilichangiwa na hali kwamba walikuwa wakichuana na Chiefs ambao chini ya kocha mpya Stuart Baxter, walikuwa wakinogesha fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia.

Ahly kwa sasa wanajivunia jumla ya mataji 22 katika soka ya CAF (Confederations Cup na Champions League) huku Chiefs wakijivunia ubingwa wa African Cup Winners Cup pekee waliounyanyua mnamo 2001.

Ingawa hivyo, kutinga fainali ya Klabu Bingwa ni ufanisi mkubwa kwa Chiefs waliokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) katika nafasi ya nane mnamo 2020-21 huku pengo la alama 31 likitamalaki kati yao na Sundowns waliotawazwa wafalme.

Al Alhy wanatarajiwa kupiga hatua zaidi katika fainali zijazo za Kombe la Dunia baada ya kukomoa  Palmeiras ya Brazil kabla ya kudenguliwa na Bayern Munich ya Ujerumani kwenye nusu-fainali mnamo 2020.Kabla ya kampeni za Kombe la Dunia kuanza, kipa Mohamed El Shenawy pamoja na wanasoka watano wengine wa Al Ahly watakuwa wamepata jukwaa maridhawa zaidi la kujinoa.

Sita hao ni sehemu ya kikosi kitakachowakilisha Misri kwenye michezo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan kati ya Julai 23 na Agosti 8, 2021.

 

  • Tags

You can share this post!

Wezi wa mifugo wauawa Samburu

Atlanta yamtimua kocha Gabriel Heinze baada ya kusimamia...