• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Zack Kinuthia afichua kuhusu mpango wa Sh5.6 bilioni kukuza vipaji vya spoti mashinani

Zack Kinuthia afichua kuhusu mpango wa Sh5.6 bilioni kukuza vipaji vya spoti mashinani

Na MWANGI MUIRURI

IKIWA mswada wa mapendekezo ya urekebishaji Katiba wa Mpango wa Maridhiano (BBI) utaishia kuwa sheria, basi kutatengwa bajeti ya Sh5.6 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya ustawishaji talanta za kispoti mashinani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Michezo Bw Zack Kinuthia, bajeti hiyo itakuwa ya kuwafaa chipukizi takribani 9, 400 ambao watapata ajira katika serikali za Kaunti wakipokezwa Sh50,000 kama mshahara wa kila mmoja wao mwisho wa mwezi.

Akiongea katika Kaunti nmdogo ya Kigumo Alhamisi katika ziara ya mawaziri Dkt Fred Matiang’i wa Usalama wa Ndani, James Macharia wa Miundombinu na Joe Mucheru wa Teknolojia, Bw Kinuthia alisema kuwa mpango maalum wa sera utawekwa rasmi.

Kisha kuwe na mkataba wa ushirikiano kati ya serikali kuu na zile za Kaunti ambao utawekwa sahihi kuongoza mpango huo.

“Ripoti ya BBI ikipitishwa katika referenda na mabadiliko ya ugavi rasilimali ambayo yanapendekezwa yaidhinishwe, ina maana kuwa tutakuwa na nyongeza za migao kwa Kaunti ambayo iatapanda kutoka asilimia 15 ya ushuru kwa sasa hadi asilimia 35. Ndani ya nyongeza hizo ndiko tunataka kutenga pesa za kufadhili mpango huu wa kutumia spoti kama njia ya kuwaundia ajira vijana wetu,” akasema.

Alisema kuwa vijana pia watanufaika kupitia kusajiliwa katika hazina za kufathili Kazi Mtaani, Ustawishaji biashara na hazina ya ustawishaji spoti mashinani ambayo kwa sasa inajumlisha Sh290 milioni na inayotazamaiwa kupanda hadi Sh360 milioni kwa mwaka ikiwa BBI itapita—zote ambazo huwa katika udhibiti wa wabunge.

Alisema kuwa hazina hizo zote zikiletwa pamoja zitakuwa na uwezo wa kuunda hazina ya takriban Sh10 bilioni kwa mwaka na mikakati iwekwe ya kuzima uwezekano wa ufisadi na mapendeleo ili kuwapiga jeki vijana kujitambua na kujiimarisha kimaisha katika hali za uwezo wao.

Katika mradi huo wa ajira kwa chipukizi wa kispoti, Bw Kinuthia alisema kuwa Kaunti zote kwa ujumla zitahitajika kuwa zikitenga Sh470 milioni kama bajeti ya kila mwezi.

“Hii ni hesabu ya Sh120 milioni kwa kila Kaunti kwa mwaka na ambapo kwa ukadiriaji wa kila Kaunti ikiwachukua vijana 200 kuwasajili katika mpango huu, tutawaundia vijana 9,400 nafasi murwa ya kuendeleza talanta zao za kispoti,” akasema.

Alisema kuwa taifa hili liko na uwezo wa kuhakikisha talanta zote mashinani haziishii kupotea katika mang’weni ya mama pima na wauzaji mihadarati kwa kukosa uwezesho ambapo mahangaiko huwasukuma kujiingiza katika uraibu wa mauti katika maisha.

“Tumekuwa tukiwasaliti vijana wetu kwa kukosa sera mwafaka ya kuwainua na hatujakuwa na ule uhalisia wa mapenzi kwa vijana wetu mashinani. Tunafaa tuunde sera maalum ya kuhakikisha vipaji vya spoti, muziki, na uigizaji vimetambuliwa, kulindwa, kukuzwa na kugeuzwa kuwa riziki,” akasema Bw Kinuthia.

Alisema kuwa talanta zitakazopewa kipaumbele katika uzinduzi wa sera hii ni soka, netiboli, voliboli, masumbwi, mpira wa vikapu na raga.

“Tutalenga kuwa kila Kaunti iunde timu zake katika safu hizo na kisha kwa ushirikishi wa serikali kuu, vijana hao wasajiliwe kushiriki ligi za Kaunti kote nchini ndio kuwe na ule mwanya wa kuhalalisha ajira na katika hali hiyo vijana hao wapate nafasi ya kutekeleza vipaji hivyo nyugani.

“Na katika hali hiyo, maskauti hata kutoka ng’ambo wanaweza wakawatambua wa kusajili katika ligi za hadhi na pesa,” akasema.

Alisema serikali kuu itakuwa ikiwapa waliosajiliwa katika mpango huu huduma za bure za kimatibabu kupitia kuwaingiza katika mpango wa bima wa NHIF ili kuwahami na uwezo wa kusaka matibabu ya hali ya juu iwapo watapata majeraha katika utekelezaji wa vipaji vyao nyugani.

You can share this post!

Nabulindo aapishwa rasmi mbunge wa Matungu

Matiang’i atoa agizo mitandao ya utapeli ivunjwe...