• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Atorosha mke wa babake akidai anamfaa

Atorosha mke wa babake akidai anamfaa

NA STEPHEN ODUOR

MWANAMUME katika Kijiji cha Magarjali, Kaunti ya Tana River, amewashangaza wakazi baada ya kutoweka na mchumba wa babake.

Babake, 71, alikuwa amenuia kumwoa binti huyo mwenye umri wa miaka 18, kama mke wa nne lakini akashtuka kutambua kuwa, mwanawe, Bw Ahmed Golo, 24, alitoroka naye.

Jamaa zake walisema, Ahmed aliwaarifu kwamba alichukua hatua hiyo kwa vile bi harusi mtarajiwa alikuwa mdogo sana kuwa mke wa babake.

Kulingana nao, alipiga simu nyumbani na kuzungumza na mama yake, akimwambia kwamba hatamruhusu babake kuwaaibisha.

Kulingana na mamake, Ahmed alisema siku za wazee kuoa wajukuu wao zilipita na kumtaka babake atafute mwanamke aliyekomaa akitaka kuoa.

“Anasema atamwoa msichana huyo na kuzaa naye kabla hajarudi nyumbani. Nilijaribu kumwambia si sawa lakini anasema msichana amekubali na anafurahi zaidi kwa kumwokoa,” akasema mamake.

Kulingana na Bw Hassan Wario, ambaye ni jamaa wa familia, mzee huyo alikuwa tayari amefanya mazungumzo na kulipa mahari ya binti huyo lakini hangeweza kumuoa kwa vile muda wa Ramadhani ulikuwa umefika.

“Alikubaliana na wazazi wa msichana huyo kuwa sherehe iliyosalia ifanyike baada ya Ramadhani, wiki ya kwanza baada ya Eid,” akasema.

Watoto kupinga ndoa

Watoto wake walikuwa wamepinga ndoa hiyo wakisema kwamba msichana huyo alikuwa na umri mdogo kuliko kitinda mimba wao.

“Tulijaribu kuongea nao lakini walikataa, hata mama zao wamejaribu kuwatuliza lakini wamekataa kabisa hasa binti zake,” akasema Bw Wario.

Baada ya vuta nikuvute kati ya baba na watoto wake, Ahmed, ambaye ni kifungua mimba wa mke wa pili, aliamua kumtafuta binti huyo nyumbani kwao, akamshawishi na wakatoroka.

Duru zinaarifu kwamba wawili hao walitoroka Jumanne alfajiri wakati jamaa wengine walikuwa katika harakati za kusali.

Waliacha barua kwa mzee huyo wakimtaka amtafute rika lake, na kuwaachia wanawe mabinti wachanga.

Jamaa za msichana huyo pia walithibitisha kuwa aliwasiliana nao akawaambia alikuwa salama.

Familia hiyo inasema kwamba, alikiri kutoridhika kwake na kuolewa na mzee, akisema ingekuwa bora aolewe na kijana.

Hata hivyo, mzee huyo amewalaumu wake zake akidai ndio walichochea watoto dhidi ya ndoa yake.

Sasa ameitaka familia ya msichana huyo kurudisha mahari na kuanza mazungumzo na mwanawe kama watakubali amwoe binti huyo.

  • Tags

You can share this post!

Miili ya watoto waliosombwa na mafuriko yapatikana

Uteuzi mwenyekiti IEBC, makamishna sita kuendelea

T L