• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mzee anayepata kibunda kwa kuchonga mashua na majahazi ya kizamani

Mzee anayepata kibunda kwa kuchonga mashua na majahazi ya kizamani

NA KALUME KAZUNGU

KWA karibu miaka 40 sasa, mzee Hassan Ali, 60, mkazi wa kisiwa cha Lamu, amekuwa akijipatia riziki kupitia uundaji na uuzaji wa modeli au miigo ya mashua, majahazi na maboti.

Baba huyo wa watoto saba alijitosa kwenye Sanaa hiyo ya kuunda modeli au miigo ya vyombo vya baharini, hasa vile vyenye asili ya Lamu, akiwa barobaro wa miaka 20 pekee.

Kilichomsukuma kujiingiza kwenye tasnia hiyo ni ufukara uliogubika familia yake na kumkosesha nafasi ya kujiendeleza kimasomo licha ya kuwa na ari ya kufanya hivyo.

Baada ya matumaini yake masomoni kufunikwa gubigubi na wingu jeusi kutokana na ukosefu wa karo, Bw Ali hakufa moyo kwani wahenga walisema ‘Ukikosa la Mama Hata La Mbwa Huamwa.’

Aliamua kujiingiza mzimamzima katika Sanaa hiyo ya kutengeneza vyombo vya baharini.

Kupitia weledi wa mjombake katika kutengeneza mashua, maboti na majahazi, Bw Ali alikaa kitako akitazama na kufuatilia kwa makini mbinu zote alizotumia mjombake kutengeneza vyombo hivyo.

Bw Ali alianza kufanyia mazoezi yale aliyokuwa akiyaona na hatimaye akaibuka kuwa mkwasi wa taaluma hiyo.

Ni wakati huo ambapo Bw Ali alipiga moyo konde na kuafikia kuanzisha karakana yake ya kutengeneza na kuuza si mashua, majahazi au maboti ya kweli bali modeli zake.

Mbali na kutumika kama virembesho nyumbani, modeli za maboti, mashua na majahazi pia hutumiwa kuwazawadi wageni wa heshima au waja waliofanya jambo la sifa na linalofaa tuzo.

Kwa sasa Bw Ali hajutii maamuzi yake ya miongo minne iliyopita kwani ni kupitia biashara hiyo ambapo hutia kibindoni hadi Sh100,000 kwa mwezi endapo wateja watajitokeza vilivyo kibandani kwake kununua bidhaa husika.

Yeye huuza modeli moja ya mashua, jahazi au boti kwa kati ya Sh1,000 hadi Sh70,000 kutegemea udogo au ukubwa wa bidhaa hizo na pia jinsi zilivyotiwa nakshi.

Mzee wa Lamu, Hassan Ali,60, ambaye anajipatia riziki kupitia uundaji na uuzaji wa modeli za mashua, maboti na majahazi. Amedumu kwenye biashara hiyo kwa miaka 40 sasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wateja wake wengi ni watalii wa ndani kwa ndani na pia wale wa kutoka mataifa ya ng’ambo.

Anasema ni kupitia biashara hiyo ambapo amefaulu kuwasomesha watoto wake saba.

Ili kuhakikisha ujuzi huo unaendelezwa kwa familia yake, kizazi hadi kingine, Bw Ali anasema tayari amewapokeza mafunzo ya kutengeneza modeli na miigo ya maboti, majahazi na mashua vijana wake wawili ambao pia wameibuka kuwa wajuzi si haba.

“Nashukuru kwamba baada ya kukosa kuendeleza masomo yangu kutokana na ukosefu wa karo, niliafikia kujitosa kwenye taaluma hii. Niliipenda tangu utotoni mwangu. Nafurahia hata zaidi kwamba Napata pesa za kukimu mahitaji ya kila siku ya familia. Nimesomesha wanangu. Pia nina furaha kwa sababu wanangu wawili wamefuata nyayo zangu. Wao ni watengenezaji mashuhuri wa modeli za maboti, majahazi na mashua,” akasema Bw Ali.

Anasema ili kuhakikisha taaluma haiangamii, yeye pia ni mkufunzi wa vijana saba wa Lamu walioonyesha hamu ya kuendeleza ujuzi huo.

“Mbali na wanangu, mimi pia nina wanafunzi saba ninaowapokeza mafunzi. Furaha yangu ni kuona taaluma hii ikiendelezwa Lamu badala ya kuachwa ipotee. Ikumbukwe kuwa mafundi wa maboti, mashua na majahazi hapa Lamu tumeachiwa sisi wazee na tuko wachache,” akasema Bw Ali.

Alipoulizwa ni wapi hasa anakotoa miti na viambata vingine vya kutengenezea modeli, Bw Ali alisema yeye huokotaokota taka zilizosheheni baharini, hasa mbao za maboti, mashua na majahazi kuukuu, plastiki, raba na vinginevyo na kuvigeuza mkutengenezea bidhaa zake.

“Mbali na biashara hii kunipatia donge nono, kwa upande mwingine pia inatunza mazingira. Kila mara huingia ufuoni kukusanya taka za plastiki, mbao, raba na vitu vingine ambavyo vikiachwa huathiri mazingira ya baharini. Husafisha vifaa hivyo na kisha kuvipiga randa na msasa na kuvifanyia kazi ya kutengeneza hizi modeli. Biashara yangu imefaulisha usafi wa ufuoni na baharini kwa jumla,” akasema Bw Ali.

Baadhi ya wateja wa Bw Ali waliozungumza na Taifa Leo walikiri kupendezwa mno na jinsi mzee huyo anavyotengeneza modeli zake kwa njia ya kipekee.

Mzee wa Lamu, Hassan Ali,60, ambaye anajipatia riziki kupitia uundaji na uuzaji wa modeli za mashua, maboti na majahazi. Amedumu kwenye biashara hiyo kwa miaka 40 sasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Isabella Jayden, mtalii kutoka Amerika anasema anapofika Lamu kujivinjari na punde anapokamilisha likizo yake, yeye hupendelea kuzuru kibanda cha mzee Ali kununua modeli anazosafirisha ng’ambo kuwapokeza wazazi wake kama zawadi.

“Hizi modeli za mashua, majahazi na maboti ya hapa Lamu ni kumbukumbu mwafaka kwamba tulifurahia ziara hapa. Mimi hununua mbili au tatu kila mwaka kupelekea wazazi wangu Amerika. Ni kitambulisho tosha kwamba Lamu ni tamu,” akasema Bi Jayden.

Justus Otieno, mtalii wa ndani kwa ndani kutoka Kisumu anasema sebule yake imesheheni modeli za mashua na maboti yanayotengenezwa na mzee Ali kisiwani Lamu.

Anasema yeye huzuru Lamu mara mbili kila mwaka na huhakikisha anakutana na mzee Ali kumueleza ni muundo gani au modeli gani ya muigo wa jahazi au mashua angetaka kutengenezewa.

“Mimi nyumba yangu iliyoko mjini Kisumu ukiingia utadhani uko Lamu. Sebule yangu imejaa hizi modeli za mashua na jahazi za Lamu na anayeniundia huwa ni mzee Ali. Nafurahia sasa hizi modeli. Ni mapambo sufufu ya nyumbani,” akasema Bw Otieno.

  • Tags

You can share this post!

Bodaboda Nakuru walazimika kubadili tabia kuwavutia wateja

Dalili zote zaonyesha Eric Omondi amejitosa katika tope la...

T L