• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Afisa wa DCI Embu atupwa ndani miaka 30 kwa makosa ya ubakaji na ulawiti

Afisa wa DCI Embu atupwa ndani miaka 30 kwa makosa ya ubakaji na ulawiti

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCIO) katika kaunti ndogo ya Manyatta iliyoko katika Kaunti ya Embu, Bw Jervasio Mwaniki Njeru mnamo Desemba 19, 2023, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na makosa ya ubakaji na ulawiti.

Bw Mwaniki, mahakama iliambiwa, alitekeleza makosa hayo kwa kumlenga mahabusu wa kike wa umri wa miaka 45 ndani ya afisi yake ya serikali miaka mitatu iliyopita.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Nairobi Bi Lucy Njuguna amemhukumu afisa huyo ambaye tayari amesimamishwa kazi, kifungo cha miaka 20 kwa makosa ya ubakaji na mingine 10 kwa kusambaratisha maadili ya afisi yake.

Hukumu hiyo sasa itamsababishia Bw Mwaniki kufutwa kazi pasipo kulipwa marupurupu yoyote.

Bw Mwaniki alikuwa awali ameachiliwa na mahakama ndogo na ndipo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ikakata rufaa katika mahakama kuu na ambapo Jaji Njuguna alisema “ilikuwa makosa kumuachilia huru mshukiwa pasipo kuzingatia hata ushahidi wa kisayansi uliokuwa umewasilishwa na upande wa mashtaka”.

“Yalikuwa makosa makuu kwa hakimu H. Nyakweba kumuachilia huru mshukiwa huyo mnamo Machi 2023, kwa madai ya ukosefu wa ushahidi hivyo basi kumsababishia mwathiriwa na mlalamishi hasara kuu katika kutafuta haki,” akasema jaji Njuguna.

Mwathiriwa alikuwa amekamatwa kwa shaka ya kutapeli Sh200,000 na afisa huyo wa DCI alisemwa kwamba alinyemelea hadi kwa seli ambapo alikuwa amezuiliwa na akamtoa na kumfululiza hadi kwa afisi yake.

Ni katika afisi hiyo ambapo afisa huyo alidaiwa kumlazimishia kitendo hicho mnamo Mei 31, 2020.

Baada ya kumfanyia unyama huo, mahakama iliambiwa na upande wa mashtaka kwamba alimuachilia huru.

Lakini mwathiriwa hakuenda nyumbani baada ya kuachiliwa bali aliingia kwa afisi ya kamanda wa kituo hicho cha polisi na akawasilisha malalamishi na ambapo Bw Mwaniki aliitwa ashuhudie ushuhuda dhidi yake.

“Bw Mwaniki aliomba msamaha na akajitolea pia kugharimia fidia pamoja na bili ya hospitali lakini msako ulifanywa na ambapo kwa kweli vazi la ndani la mwathiriwa lilipatikana ndani ya afisi ya Bw Mwaniki pamoja na karatasi shashi iliyotumika,” mahakama ikaambiwa.

  • Tags

You can share this post!

UDAKU: Milly Chebet asusia oparesheni ya kupunguza unene

Picha za maudhi kwa mke wa wenyewe zamfikisha mwanamume...

T L