• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Chiloba atisha kuzima vituo 60 vya redio

Chiloba atisha kuzima vituo 60 vya redio

Na CHARLES WASONGA

TUME ya Mawasiliano (CA) imetisha kufutilia mbali leseni za kuhudumu na masafa zilizopewa vituo 60 vya redio nchini.

Kupitia tangazo la kulipiwa lililochapishwa katika ukurasa wa tisa katika gazeti la Daily Nation, toleo la Desemba 22, 2021, mkurugenzi mkuu wa tume hiyo Ezra Chiloba alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya vituo hivyo kufeli kuzingatia masharti yaliyowekwa kwenye leseni hizo.

“Zingatia kwamba tume hii imeanzisha utekelezaji wa hatua dhidi ya vituo vya redio na waliowasilisha maombi ya leseni kwa kufeli kuzingatia masharti kuhusu utoaji leseni inavyohitajika kisheria,” akasema Bw Chiloba bila kutaja moja kwa moja masharti ya leseni hizo.

Baadhi ya vituo vya redio vilivyoathirika ni pamoja na; Capital FM, NRG, Mbaitu FM, Redio Umoja, KU 99.9 FM, Radio Furaha, Wendo FM miongoni mwa vingine. Kulingana na mkurugenzi huyo mkuu wa CA, taarifa kuhusu uamuzi huo imetumwa kwa vituo husika kwa redio kwa maandishi.

Vituo hivyo, vimepewa muda wa siku 30 kuzingatia mahitaji hayo jinsi yalivyoratibiwa. “Ukiukaji wa hitaji hili utavutia adhabu ya faini ya kiwango kisichopungua Sh1 milioni au kifungo cha miaka mitatu gerezani au adhabu zote mbili,” Bw Chiloba akasema kwenye taarifa hiyo.

You can share this post!

Elgon Kenya na UoN kushirikiana kuanzisha mafunzo ya...

Waliofariki kimbungani Ufilipino sasa wafika 375

T L