• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Waliofariki kimbungani Ufilipino sasa wafika 375

Waliofariki kimbungani Ufilipino sasa wafika 375

Na AFP

MANILA, Ufilipino

IDADI ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Rai nchini Ufilipino jana ilifika 375, kulingana na takwimu zilizotolewa na polisi.

Watu wengine 500 waliripotiwa kujeruhiwa huku 56 wakisemekana hawajulikani waliko.Msemaji wa polisi alisema kuwa kwa ujumla kimbunga hicho kiliwaacha jumla ya watu 400,000 bila makao na wakalazimika kukimbilia usalama katika visiwa vya kusini mwa Ufilipino.

Nayo makundi ya uokoaji yalisema ilikuwa vigumu kubaini hasara iliyosababishwa na kimbunga Rai kilichovuma kwa kasi ya kilomita 195 kwa saa.Jana, kulikuwa na hofu kwamba mvua iliyosababishwa na kimbunga hicho ingesababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko.

Hali hiyo, maafisa wa usalama walisema, huenda ikasababisha maafa zaidi.Wakati huo huo, idadi ya watu waliofariki katika mkasa wa mafuriko nchini Malaysia jana ilifika 14 huku zaidi ya watu 70,000 wakipoteza makao.Wanajeshi walitumia maboti kusambaza chakula kwa watu waliokwama katika nyumba zao kufuatia mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Mvua hiyo ilianza kunyesha kote nchini Malaysia na kusababisha mafuriko makubwa mijini na vijijini na kuharibu barabara zote kuu.Jimbo la Selangor – lenye idadi kubwa ya watu na linalopakana na jiji kuu la Kuala Lumpur, ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi.

Katika jiji la Shah Alam, baadhi ya maeneo bado yalikuwa ndani ya maji kufikia jana asubuhi.Kartik Subramany alihama nyumba yake na kusaka hifadhi katika shule moja kwa saa 48 baada ya kuhamishwa, pamoja na familia yake, katika hema fulani.

“Nyumba yangu imeharibiwa kabisa, magari mawili yaliharibiwa kabisa,” mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 29 aliambia AFP. “Haya ni mafuriko mabaya zaidi kushuhudia maishani mwangu. Serikali ya majimbo imefeli kutekeleza wajibu wake wa kulinda maisha ya raia”Mbunge wa upinzani Fuziah Salleh alikosoa hatua ambazo serikali ilichukua kuokoa wahanga wa mafuriko hayo akizitaja kama “zisizo na manufaa yoyote.”

“Serikali ilifeli kabisa kutoa onyo mapema kwamba mvua kubwa ingenyesha. Ni huzuni kuwa watu wamefariki,” mbunge huyo akasema.Miongoni mwa watu 14 waliothibitishwa kufariki jana, wanane wanatoka Selangor na sita wanatoka mashariki mwa jimbo la Pahang, kulingana na ripoti za shirika la habari la Bernama.

Idadi ya waliofariki inatarajiwa kupanda ikizingatiwa kuwa kuna watu ambao bado hawajulikani waliko.Malaysia hukumbwa na mafuriko kila mwaka lakini mafuriko ya wikendi iliyopita yametajwa kuwa mabaya zaidi tangu mwaka wa 2014.

Katika mwaka huo, zaidi ya watu 100,000 walilazimisha kutoroka makwao.Ongezeko la viwango vya joto limehusishwa na mikasa ya mafuriko. Kwa sababu anga lenye joto husheheni maji mengi, mabadiliko ya hali ya anga huongeza uwezekano wa mvua kubwa kunyesha.

You can share this post!

Chiloba atisha kuzima vituo 60 vya redio

Duale aapa kupinga Mswada wa miungano ya kisiasa

T L