• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Hakimu aeleza kusikitishwa kwake huku akiachilia Rotich na wenzake katika wizi wa Sh63 bilioni

Hakimu aeleza kusikitishwa kwake huku akiachilia Rotich na wenzake katika wizi wa Sh63 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI

ILIKUWA furaha na kilio katika mahakama ya Milimani pale aliyekuwa waziri wa fedha Henry Rotich na watu wengine nane walipoponyoka vifungo vya miaka na mikaka katika kashfa ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kwa gharama ya Sh63 bilioni.

Bw Rotich alidondokwa na machozi sawia na washtakiwa wenzake hakimu mkuu Eunice Nyuttu aliposema “Hakuna ushahidi uliowasilishwa kuwezesha mahakama kuwasukuma kizimbani kujitetea.”

Bi Nyuttu alikashifu afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma DPP kukwepa majukumu yake na kutowasilisha ushahidi kutoka kwa mashahidi 41 akiwamo waziri wa zamani wa kilimo Peter Munya.

“Viongozi wa mashtaka waliambia hii mahakama-hatuna maswali kwa mashahidi hawa 41 kati ya mashahidi 49,” alisema Bi Nyuttu.

Hakimu alisema DPP alikosa kutumia ipasavyo mamlaka aliyopewa katika kifungu 157 cha katiba na kuletea mahakama na umma wa Kenya fedheha.

Akiwaachilia Bw Rotich huru, hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kei za ufisadi Bi Eunice Nyuttu alisema “upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka 19 dhidi ya washtakiwa.”

“Hakuna ushahidi uliowasilishwa katika kesi hii kuthibitisha upunjaji wa zaidi ya Sh63 bilioni dhidi ya washtakiwa wote,” alisema Bi Nyuttu.

Hakimu huyo aliwakashfu viongozi wa mashtaka aliosema “walihepa kesi hiyo na kukataa kuwasilisha ushahidi wa mashahidi 41.”

Akasema Bi Nyuttu:“Wakati kiongozi wa mashtaka Taib Ali Taib alipotoa taarifa yake ya kwanza alisema ushahidi utawasilishwa kuthibitisha jinsi washtakiwa walikula njama za kuipunja serikali Sh80 bilioni katika kashfa hiyo ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.”

Akimnukuu Bw Taib, Bi Nyuttu alisema kiongozi huyo wa mashtaka alisema “upande wa mashtaka utathibitisha jinsi kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa ilishinda tenda ya ujenzi wa mabwawa hayo mawili ya Arror na Kimwarer.”

Hakimu alieleza kiongozi huyo wa mashtaka alisema ushahidi wa kushtua utawasilishwa jinsi pesa za umma zilianza kulipwa hata kabla ya ujenzi wa mabwawa hayo kuanza.

Bi Nyuttu alisema baada ya mashahidi wanane kutoa ushahidi viongozi wa mashtaka walianza kukwepa kuwasilisha ushahidi kwa lengo la “kutafuta jinsi washtakiwa wataachiliwa huru na mahakama.”

Hakimu alisema tabia hii ya viongozi wa mashtakiwa ilifedhehesha mahakama na washtakiwa aliosema wamekuwa kortini kwa muda mrefu wakisubiri kupata haki.

Lakini hakimu alisema washtakiwa waliowakilishwa na mawakili Kioko Kilukumi, Katwa Kigen na Philip Nyachoti “hawakutendewa haki kamwe ila viongozi wa mashtaka walianza mchezo wa paka na panya kwa kuleta mashahidi na kutowauliza maswali.”

Katika kesi hiyo, Bw Rotich alishtakiwa pamoja na Nyakundi Nyachiro, Jackson Njau Kinyanjui, David Kipchumba Kimosop, William Kipkemboi Maina, Paul Kipkoech Serem, Francis Chepkonga Kipkech, Titus Muriithi na Geoffrey Mwangi Wahungu.

Walikabiliwa na mashtaka ya kutumia mamlaka ya afisi zao vibaya katika ujenzi wa Arror na Kimwarer.

Washtakiwa hao tisa walikana shtaka la pamoja la kula njama za kuilaghai Serikali ya Kenya Dola za Marekani ($) 501,829,769 kwa kuidhinisha ujenzi wa mabwawa haya ya Kimwarer na Arror kabla ya kujadiliwa na kupitisha na asasi husika za serikali.

Walishtakiwa kuzipa kampuni za Italia ujenzi wa miradi hiyo kinyume cha sheria.

Hakimu alisema kampuni hizo Cooperativa Muratori & Cementisti (CMC di Ravenna) na Itinera S.p.A zilipewa kandarasi hiyo.

Mahakama ilisema hoja kuhusu kandarasi hiyo ziliibuka na zabuni hiyo ikapigwa kalamu ndipo serikali ikashtakiwa katika jopo la kimataifa na kampuni hizo.

Kampuni hizo ziliomba zilipwe kitita cha Sh80 bilioni.

Mahakama ilisema mamlaka ya KVDA ilitoa idhini ya ujenzi huo iliyosema haukuwa umesukwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo mahakama ilisema afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma haikuwasilisha ushahidi kuthibitisha mashtaka 19 dhidi ya washtakiwa iliowaachilia huru.

Bi Nyuttu aliamuru washtakiwa warudishiwe dhamana zao.

Pia aliamuru uamuzi wake upelekewe asasi husika za serikali zikajadili njia za kuwaadhibu viongozi wa mashtaka waliokwepa kesi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Amerika yaanza kunawa mikono kuhusu vita vya Israel ukanda...

Unaringa na ni Karen Nyamu amekusaidia kupata tuzo,...

T L