• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Idadi ya wanaotumia ARVs yapanda kwa asilimia 83 – Rais

Idadi ya wanaotumia ARVs yapanda kwa asilimia 83 – Rais

ERIC MATARA na COLLINS OMULLO

IDADI ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa wa Ukimwi imeongezeka kwa asilimia 83.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka watu 656,000 hadi milioni moja ndani ya muda wa miaka miwili iliyopita.

Akiongea Jumatano alipoongoza sherehe za kitaifa za Kuadhimisha Siku ya Ukimwi Ulimwenguni mjini Nakuru, Rais Uhuru Kenyatta, aliiagiza Wizara za Afya na Fedha kufanikisha ununuzi wa dawa hizo pamoja na bidhaa zingine za kukabili ugonjwa huo.

“Kila mwaka Kenya huhitaji Sh25.4 bilioni kununua bidhaa za kupambana na Ukimwi. Hizi ni kama vile dawa za ARVs pamoja na vifaa vya kubaini uwepo wa virusi vya ukimwi mwilini mwa mwanadamu,” akasema, katika uwanja wa Nakuru Athletics Club.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alisema changamoto katika ufadhili wa mipango ya tiba ya Ukimwi imesababisha mahangaiko kwa karibu watu 1.5 milioni wanaoishi na Ukimwi nchini.

“Ni kwa msingi huu ambapo naamuru Waziri wa Afya na mwenzake wa Fedha kufanya kazi kwa pamoja kusaka suluhu kwa changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaa vya kudhibiti makali ya janga hili,” kiongozi wa taifa akakariri.

Rais Kenyatta pia alisema badala ya Kenya kutegemea ARVs na vifaa vya Ukimwi vinavyoagizwa kutoka mataifa ya kigeni, ipo haja ya bidhaa hizo kununuliwa humu nchini.

“Sharti Kenya itafakari kuhusu uwezekano wa kushirikiana na kampuni za humu nchini kufanikisha utengenezaji wa vifaa vya kudhibiti Ukimwi. Hii ndio njia itakayohakikisha watu wanaoishi na ugonjwa huu wanapata usaidizi haraka na kwa gharama nafuu,” akaeleza.

Rais Kenyatta alisema ili kufanikisha ndoto hiyo, Serikali yake inataketeleza mpango wa kuifanyia mageuzi Mamlaka ya Dawa Nchini (Kemsa).

“Baada ya mageuzi hayo kukamilika, asasi hiyo itaweza kusambaza bidhaa hizi bila changamoto zozote. Sharti tuendeleze mafanikio ambayo tumeandikisha katika vita vya kuangamiza janga hili,” akaeleza.

Alisema kuwa juhudi hizi za kupambanana na Ukimwi zinaweza tu kuzaa matunda ikiwa watu wataepukana na ngono za kiholela.

Rais Kenyatta alisema tabia ya wazee kushiriki ngono na wasichana wadogo imechochea ongezeko la visa vya maambukizi ya maradhi ya zinaa ikiwemo Ukimwi.

“Wanaume wazima wakome kushiriki ngono na wasichana wadogo. Tuheshimu kizazi hiki kwa kutowaambukiza maradhi ya zinaa, Ukimwi au mimba za mapema. Hawa watoto ndio kesho yetu; tafadhali tusiwaharibu,” akasisitiza.

Wakati huo huo, vijana wa umri wa miaka 15 na 24 wanaongoza kwa maambukizi ya virusi vya HIV na Ukimwi, jijini Nairobi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Idara za Huduma Jijini Nairobi (NMS) Mohamed Badi alisema kuwa asilimia 40 ya maambukizi mapya jijini yanahusisha vijana wa umri huo.

Watu 167,447, wanaishi na virusi vya HIV jijini Nairobi kulingana na Jenerali Luteni Badi.

Jiji la Nairobi linashikilia nafasi ya saba kwa idadi ya juu ya maambukizi nchini.

Kasi ya maambukizi ya virusi vya HIV iko juu miongoni mwa vijana wa kike kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na wenzao wa kiume asilimia 3.3  .

Wakati huo huo, Badi alisema wasichana 4,932 wa kati ya umri wa miaka 10 na 14 walipata mimba kati ya Januari 2020 na Septemba 2021.

You can share this post!

TAHARIRI: Ya Mwendwa yameisha, tuboreshe soka sasa

Kinaya cha Kenya tajiri bila senti mifukoni

T L