• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Jamhuri kavu, Wakenya wakiendelea ‘kusota’

Jamhuri kavu, Wakenya wakiendelea ‘kusota’

NA BENSON MATHEKA

WAKENYA Jumanne, Desemba 12, 2023 wameadhimisha miaka 60 ya kujitawala bila matumaini huku wakilemewa na gharama ya maisha, ukosefu wa ajira, kukabiliwa na njaa, maradhi na kushindwa kulipia karo watoto wao kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Kwa vijana kote nchini ambao ndio asilimia 75 ya raia wa Kenya, uhuru kwao ungali ndoto huku hata waliosoma hadi vyuo vikuu wakishindwa kupata riziki.

Wataalamu wanasema kwamba Kenya haina uwezo wa kulisha raia wake kwa namna toshelevu miaka 60 baada ya kujikomboa kutoka ukoloni.

Njaa ni mojawapo ya maadui watatu wakuu ambao rais mwanzilishi wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta na serikali yake aliazimia kuangamiza.

Maadui wengine wawili ni maradhi na kutojua kusoma na kuandika.

Bw Timothy Njagi, mtafiti katika Tegemeo Institute of Agriculture Policy and Development anasema kwamba kuna watu wengi wanaolala njaa nchini Kenya hata katika maeneo ya mijini; idadi ambayo imeongezeka miaka michache iliyopita kwa sababu ya janga la Covid-19, ukame na hali ya sasa ya mfumko wa bei za vyakula huku mapato yakipungua.

“Tatizo pia linatokana na ukweli kwamba watu wengi katika maeneo ya miji hawapandi chakula na kwa hivyo, wanapokosa mapato ya kununua, hulazimika kupunguza mlo,” asema Njagi.

Ingawa ndoto ya Mzee Jomo Kenyatta ilikuwa kuwawezesha Wakenya maskini kupitia elimu, kupata elimu hiyo kumebaki kuwa ndoto huku wengi wakishindwa kumudu karo ya watoto wao.

“Kama ilivyo katika Ripoti ya Ominde ya 1964, Rais wa zamani alitaka kutumia elimu kuwawezesha Wakenya kiuchumi, kuunganisha na kukuza umoja wa kitaifa. Miaka 60 baadaye, tumepiga hatua za ajabu kulingana na maono ya Ominde ikiwa ni pamoja na maendeleo ya teknolojia na ufahamu wa kimataifa,” akasema mhadhiri mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi Dkt Julius Jwan.

Hata hivyo, wanaosoma hadi vyuo vikuu hawapati ajira na wanaofanya vibarua wanalemewa na gharama ya juu ya maisha inayoshuhudiwa nchini kwa wakati huu.

Sera za serikali ya sasa ya Kenya Kwanza zinaonekana kuenda kinyume na ndoto ya waanzilishi wa taifa la Kenya za kuwezesha raia kuwa na maisha bora kuliko waliyokuwa nayo chini ya utawala wa kikoloni.

Serikali imekumbatia mikopo kutoka mashirika yanayodhibitiwa na nchi za Ulaya yanayotoa masharti makali yanayoumiza raia wa kawaida kwa kumbebesha mzigo mkubwa wa ushuru.

“Kwa mujibu wa takwimu, Kenya inakabiliwa na tatizo la ongezeko la vijana, huku makadirio yakionyesha kuwa asilimia 75 ya wakazi wa Kenya wana umri wa chini ya miaka 35.

Ukosefu wa ajira kwa vijana nchini unasemekana kuwa juu hadi asilimia 35 (takriban vijana na wanawake milioni 4.5 hawana ajira), ikilinganishwa na kiwango cha ukosefu wa ajira kitaifa cha asilimia 10.

Katika mwaka mmoja uliopita, Wakenya kadhaa wamepoteza kazi.

Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) lilishutumu kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji nchini, huku likionya kuwa maelfu ya Wakenya watakosa kazi iwapo sera za serikali kuhusu ushuru hazitabadilishwa.

 

  • Tags

You can share this post!

Serikali ya Sakaja yaachilia mwili wa aliyegongwa akihepa...

Wakazi walivyosaidia polisi kuua wezi, na kuokoa mbuzi 1,600

T L