• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
Jiandae kwa maandamano, Karua aambia serikali akiiponda kuhusu gharama ya maisha

Jiandae kwa maandamano, Karua aambia serikali akiiponda kuhusu gharama ya maisha

NA FRIDAH OKACHI

KIONGOZI wa Chama cha Narc Kenya Martha Karua ametishia kurejesha Wakenya barabarani iwapo serikali haitasikiza matakwa ya Azimio kuhusu gharama ya maisha.

Bi Karua alisema muafaka wa mazungumzo yaliyofanyika Bomas huenda usipatikane, iwapo serikali itashikilia msimamo kuwa gharama ya maisha si suala la dharura.

Akizungumza Alhamisi, Novemba 16, 2023 katika makao makuu ya chama cha Narc Kenya jijini Nairobi, Bi Karua alisema gharama ya maisha iko juu, lakini serikali badala yake inaendeleza mipango iliyo na kashfa za ufisadi.

Alidai Rais William Ruto amekuwa akiwateua wale wanaokabiliwa na mashataka ya ufisadi na kuamrisha Afisi ya Mkurungezi wa Mashataka kuondoa kesi hizo.

“Jambo la kwanza serikali imepuuza Katiba na sheria za Kenya. Hali hii imezidi. Watumishi wa umma wanaokabiliwa na uhalifu, kesi zao zinaondolewa na kupewa kazi katika afisi za umma,” alisema Bi Karua.

Alilaumu Kiongozi wa Mashtaka kuhujumu kesi za ufisadi na kukosa kutoa ushahidi wowote dhidi ya maafisa wakuu wanaokabiliwa na uhalifu.

“Tunakumbuka vizuri kesi ya mabwawa ya Kimwarer na Arror. Walitoa hati ya kukamwatwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya kukosa kwenda kutoa ushahidi, ilhai upande wa mashtaka haukuwa umemfahamisha. Bw Munya alijipeleka mahakamani na kusema yupo tayari kutoa ushahidi na kiongozi wa mashtaka alisema hana maswali ya kumuuliza. Kesi nyingi zinahujumiwa na wanaowekwa huru ni wanatoka jamii ya Rais,” aliendelea.

Alikashifu vitisho vinavyotolewa na Rais William Ruto kuwa ‘Mambo ni Matatu’ akisema ni tishio la kuuawa kwa raia kwa njia isiyoeleweka.

“Hili ni tishio la kuua kutoka kwa Bw Ruto. Jambo la pili ni kuondoa kesi mahakamani. Shinikizo ya aina hii haikubaliki,” alisema Bi Karua.

Vile vile, alimtetea mfanyabiashara Ann Njeri, kwenye sakata ya kutoweka kwa mafuta ya Sh17 bilioni, akisema kutekwa nyara ilikuwa njama ya serikali kuingilia ushahidi.

“Mfanyabiashara huyu hajulikani. Sijui mafuta hayo ni ya nani. Serikali haitaki tujue ni nani anamiliki?” alisema.

Alidai kuwepo ubaguzi katika ufadhili wa elimu na kutaka elimu ya shule za msingi na sekondari ifadhiliwe vilivyo.

Alisema ni kwa njia hiyo ambapo viwango vya elimu nchini vitarejeshwa mahali pake kama awali, ili kuepuka wanafunzi kusalia nyumbani.

“Suala la unga ni muhimu lakini pia elimu hapa nchini inadunishwa. Tunataka kuona ufadhili wa wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia mikopo kwa wanafunzi. Wanafunzi wote wapokee mkopo huo na si kubagua jinisi serikali ya Kenya kwanza inataka kuazisha, tunakataa kubaguliwa kwa kila njia,” alisema Bi Karua.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yatangaza kusimamisha kazi maafisa wakuu sita wa...

Haiya, sikujua binti yangu ni tajiri hivi, asema mamake...

T L