• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Serikali yatangaza kusimamisha kazi maafisa wakuu sita wa mashirika, mhasibu kwa ufisadi

Serikali yatangaza kusimamisha kazi maafisa wakuu sita wa mashirika, mhasibu kwa ufisadi

Na FATUMA BARIKI

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei ametangaza kwamba maafisa sita wakuu wa mashirika ya kiserikali, mhasibu na maafisa 67 wa polisi wamesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, Mkuu huyo wa Utumishi wa Umma ameeleza kwamba wamepokea mapendekezo kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Tanathi Fredrick Mwamati ni wa kwanza kupendekezwa asimamishwe kazi, kulingana na ombi lililotumwa kwa Waziri wa Maji na Unyunyuziaji Zachariah Njeru. Bw Mwamati ambaye ni mhandisi anashukiwa kuhusika na utoaji zabuni kwa njia ya kifisadi kwenye mradi wa usambazaji maji wa eneo la kibiashara la Leather Industrial Park.

Wa pili ambaye Waziri wa Leba Florence Bore anashauriwa kumsimamisha kazi ni Stephen Ogenga, ambaye ni mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Kitaifa ya Kiviwanda (NITA) kwa tuhuma za ufisadi katika ununuzi na utoaji zabuni.

Vile vile, Stanvas Ong’alo ambaye ni kaimu mkurugenzi mkuu wa Makavazi ya Kitaifa amesimamishwa kazi kwa tuhuma za wizi wa Sh490 milioni.

Naye Bw Benjamin Kai Chilumo wa Huduma Centre ambaye yuko chini ya Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, ameambiwa aache kazi mara moja kutokana na madai ya kuhusika katika wizi wa pesa alipokuwa anahudumu kama Afisa Mkuu wa Fedha katika Kaunti ya Kilifi.

Mwingine aliyesimamishwa kazi ni Afisa Mkuu wa Bomas Of Kenya, Peter Gitaa Koria, ambaye anatuhumiwa kushiriki ununuzi visivyo kwenye shirika lake hilo ambalo limo chini ya Waziri Aisha Jumwa.

Vilevile, Anthony Wamukota ambaye ni Meneja Msimamizi wa kitengo cha Ubunifu na Ujenzi katika KETRACO amesimamishwa kazi kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma katika ujenzi wa Kituo cha kuzalisha nguvu za umeme cha 400KV Loiyangalani.

Esther Wanjiru Chege ambaye ni mhasibu wa shirika la KeRRA pia amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuwa na utajiri usioelezeka.

Aidha, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome ametakiwa kuachilia maafisa 67 ambao wamehusishwa na ufisadi.

EACC inasema kwamba kuendelea kuwepo kwa maafisa hao kazini kutahujumu uchunguzi na mashtaka yanayowakabili.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi kuumia upya kaunti ikiongeza ada ya kuwakusanyia...

Jiandae kwa maandamano, Karua aambia serikali akiiponda...

T L