• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 6:55 AM
Kalonzo alaani ubomoaji katika mtaa wa Mukuru

Kalonzo alaani ubomoaji katika mtaa wa Mukuru

Na CECIL ODONGO

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka amelaani ubomoajii ambao umekuwa ukiendelea katika mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga viungani mwa jiji la Nairobi, akisema haujakuwa ukiendeshwa kwa kuzingatia ubinadamu.

Bw Musyoka alisema kuwa ni kinaya kwa serikali yenye jukumu la kulinda maslahi ya Wakenya kwenda kinyume na matarajio hayo.

Alisema Rais Uhuru Kenyatta aliapa kulinda maslahi ya Wakenya aliposhika hatamu za uongozi ilhali sasa ni utawala wake unaoendelea kusambaratisha maisha ya watu hao.

Akizungumza baada ya kusambaza vyakula kwa waathiriwa wa ubomozi huo, Bw Musyoka alisema shughuli hiyo imekuwa ikichochewa na baadhi ya watu ambao wanalenga kunyakua ardhi hiyo.

“Wanyakuzi hao wa ardhi wanatumia suala la barabara kupitia mtaa huo kupata vipande vya ardhi vya kustawisha. Nitayawasilisha malalamishi ya wahasiriwa hao kwa Rais Uhuru Kenyatta ili wapewe makao mapya,” akasema Bw Musyoka.

Aidha alisema serikali inafaa iombe msamaha kwa wakazi wa Mukuru kwa Njenga kutokana na kupigwa risasi na mauaji yaliyotokea akikariri kuwa ni wajibu wa serikali kulinda maisha ya raia wala si kuwaua.

Alikuwa ameandamana na mbunge wa eneo hilo Musili Mawathe, wabunge Makali Mulu, Jessica Mbali na Joshua Mwalyo kati ya wanasiasa wengine wa Wiper.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais atimize ahadi ya kuilinda mipaka yetu

Pesa za wanachama wa Sacco katika hatari ya kuibwa

T L