• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kindiki: Maafisa wamevunja majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa

Kindiki: Maafisa wamevunja majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa

NA GEOFFREY ONDIEKI

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amesema ‘Operesheni Maliza Uhalifu’ Kaskazini mwa Bonde la Ufa imefanikiwa licha ya ripoti za mashambulio makali ya majangili na majambazi katika eneo hilo.

Waziri huyo alisema Jumatano kuwa vikosi vya usalama kutoka vitengo mbalimbali vinavyoongoza operesheni hiyo katika maeneo ya Samburu, Baringo, Laikipia, Turkana, na Elgeyo Marakwet vimeweza kukomesha majambazi maeneo ya kaskazini mwa Bonde la Ufa.

Kauli ya Bw Kindiki inajiri licha ya ripoti kadhaa za mashambulio ya majambazi katika eneo la Samburu Magharibi na sehemu za Baringo Kaskazini.

“Tumepiga hatua kubwa katika kukomesha ujambazi katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa,” waziri Kindiki alisema katika taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Ujambazi katika sehemu kubwa ya Kaunti ya Samburu umedhibitiwa kwa mafanikio makubwa, hasa huko Baragoi, kitovu cha uhalifu,” aliongeza.

Prof Kindiki mnamo Jumatano asubuhi alizuru Kaunti ya Samburu kutathmini hali ya operesheni za usalama zinazoendelea.

Hata hivyo, katika mkutano huo wa usalama ambao ulifanyika Kisima eneo la Samburu Magharibi, wanahabari walizuiwa kuangazia mkutano huo.

“Hamruhusiwi kuangazia mkutano huu,” alisikika akisema mmoja wa maafisa wa usalama.

Waziri huyo alisema serikali inaendelea kufuatilia mafanikio na changamoto za operesheni ya usalama inayoendelea katika kaunti zote zilizokumbwa na visa vya utovu wa usalama, ambazo ziliorodheshwa kuwa “hatari.”

Hatua hiyo, kulingana na Bw Kindiki, itasaidia kukabiliana na changamoto ya mpango endelevu wa kutokomeza ugaidi wa wezi wa mifugo wenye silaha ambao wamesababisha mauaji na wizi wa mali ya Wakenya wasio na hatia kwa miongo kadhaa.

“Miezi minane ya vikosi vya Operesheni Maliza Uhalifu sehemu hii, serikali inaendelea kufuatilia mafanikio na changamoto za operesheni,” alisema waziri.

“Serikali imejitolea kuendeleza Operesheni ya Maliza Uhalifu kwa kutokomeza kabisa ujambazi na wizi wa mifugo Kaskazini mwa Kenya,” aliongeza.

Baadhi ya maeneo ya Samburu Magharibi bado yana hali tete miezi minane baada ya kutumwa kwa vikosi vya usalama kudhibiti ujambazi katika eneo hilo.

Wenyeji waliozungumza na Taifa Leo Jumatano walisema majambazi waliojihami bado wanazurura kwenye mapango na korongo katika maeneo yenye matatizo.

Ripoti zinaonyesha kuwa wahalifu bado wanaishi katika mapango na korongo, ambako wanatumia kupanga na kutekeleza shughuli za ujambazi. Eneo hili linakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya majambazi ambayo sio tu yamevuruga familia, lakini pia yamevuruga shughuli za kielimu, shughuli za kiuchumi na utoaji wa huduma za kawaida.

  • Tags

You can share this post!

Jibaba lalia kilabuni baada ya vipusa kulinyima burudani

Siri ya kumudu Karatasi ya Pili ya KCSE Kiswahili kama...

T L