• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Krismasi: Wewe ndiye umesota! Wengine wanaponda raha

Krismasi: Wewe ndiye umesota! Wengine wanaponda raha

JURGEN NAMBEKA, KEVIN CHERUIYOT na MERCY SIMIYU

MAELFU ya watu kutoka sehemu tofauti nchini wanasafiri kuelekea maeneo mbalimbali kufurahia msimu huu wa sherehe, na kuuaga mwaka ambao umekuwa mgumu kiuchumi.

Wakionekana kutotishika, wengi wao wako tayari kuukumbatia msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya ili kujenga kumbukumbu za kudumu maishani mwao.

Uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali katika miji mingi mikubwa nchini, ulibaini kuwa kuna ongezeko la shughuli nyingi katika sekta ya uchukuzi kwa njia kama reli, barabara au hata anga.

Katika eneo la Pwani kwa mfano, mikahawa mingi imejaa wageni hasa jijini Mombasa na Diani kutokana na idadi kubwa ya watu waliofika kwa sherehe hizo.

Wenye vyumba vya malazi, maarufu kama Airbnb, wameongeza ada zao kwa hadi mara mbili.

Jaribio la wanahabari wa Taifa Leo Dijitali kukata tiketi kwenye kampuni kubwa za mabasi, mashirika ya ndege na gari la moshi la Madaraka (SGR), liligonga mwamba, kwani zimejaa hadi Siku ya Krismasi.

Hakuna nafasi yoyote iliyobaki hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Kwa mfano, mabasi ya kampuni ya Easy Coach kutoka Nairobi hadi Kisumu yamejaa hadi Desemba 24, huku yale ya kampuni ya Mash kutoka Nairobi hadi Kisumu, na Mombasa hadi Kisumu pia yalijaa kabisa hadi kesho, Jumapili, Desemba 24.

Kampuni ya Easy Coach imeimarisha huduma zake za uchukuzi kwa kuongeza mabasi mengine 12 zaidi.

Kampuni hiyo, ambayo huhudumu kati ya Nairobi hadi Magharibi mwa Kenya na Nyanza iliongeza nauli zake kwa Sh100.

“Uamuzi wetu wa kuongeza nauli zetu kwa kiwango kidogo unalenga kuhakikisha hatuwafinyilii sana wateja wetu. Maeneo tunayohudumu kwa wingi ni Nyanza ya Kati, Magharibi na Nyanza Kusini. Tunahakikisha kuwa madereva wetu wanazingatia kikamilifu sheria na kanuni za barabarani. Watahudumu tu kwa hadi saa kumi ili kuhakikisha wanazingatia usalama barabarani,” akasema Bw Dennis Ouma, ambaye ndiye Meneja Mkuu wa Kituo cha Mabasi cha Easy Coach.

Reli ya SGR, ambayo Wakenya wengi hupenda sana kuitumia kama njia ya haraka na nafuu ya usafiri, pia imejaa.

Nafasi za usafiri kati ya Nairobi na Mombasa zitaanza kupatikana Desemba 30.

Mashirika ya ndege pia yanavuna pakubwa msimu huu wa sherehe kutokana na idadi kubwa ya watu ambao wanasafiri.

Katika shirika la ndege la Jambojet, juhudi za kikosi cha shirika la habari la Nation kukata tiketi za kusafiri kutoka Kisumu hadi Mombasa hazikufua dafu, baada yao kubaini kuwa nafasi zote za usafiri zimejaa hadi Desemba 30.

Ni nafasi chache tu zilizopo za watu wanaosafiri kutoka Nairobi hadi Mombasa, kwani Sikukuu ya Krismasi 2023 inaendelea kukaribia.

Vivyo hivyo, huduma za usafiri katika shirika la ndege la Skyward pia zinatafutwa na watu wengi.

Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ) lililazimika kuongeza ndege moja zaidi ili kushughulikia idadi kubwa ya wasafiri katika msimu huu wa sherehe.

Shirika hilo lilisema kuwa lilikodisha ndege aina ya A330 Airbus kutoka shirika la Hi Fly kutoka nchini Ureno.

Ndege hiyo ina uwezo kubeba abiria 229.

“Kutokana na ongezeko kubwa la wasafiri, tumelazimika kuongeza ndege moja zaidi ili kukidhi mahitaji yao ya usafiri.Kutokana na uwepo wa ndege hiyo, tunatarajia kuimarika kwa huduma za usafiri miongoni mwa abiria wetu,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo, Bw Allan Kilavuka, kupiitia taarifa.

Mabasi yanayosafiri kutoka Nairobi hadi Kisumu, Kitale, Bungoma, Eldoret na Busia, yanatoza abiria nauli ya Sh2, 000 kutoka Sh1, 700 huku wale wanaoelekea Kisii wakitozwa Sh1, 600.

Katika nyakati za kawaida, abiria wanaosafiri hadi Kisunu, Eldotet na Kitale huwa wanatozwa kati ya Sh1, 000 na Sh1, 400.

 

  • Tags

You can share this post!

Wabunge walalamikia visa vya watu kutoweka

Kanisa lasisitiza umuhimu wa elimu ya ngumbaru kuzima...

T L