• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Kanisa lasisitiza umuhimu wa elimu ya ngumbaru kuzima uhasama Turkana

Kanisa lasisitiza umuhimu wa elimu ya ngumbaru kuzima uhasama Turkana

NA LAWRENCE ONGARO

KANISA la Glory Outreach Assembly (GOA) la Kahawa Wendani, limezindua mahamasisho ya kuhimiza watu wazima kukumbatia elimu katika jamii.

Kanisa hilo lilituma ujumbe kuzuru Kaunti ya Turkana.

Kulingana na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, lengo lao kuu ni kuona ya kwamba wanawahamasisha watu wazima kwa lengo la kuwashauri waachane na wizi wa mifugo unaotekelezwa mara kwa mara.

“Juhudi zetu zilizalisha matunda ambapo wanafunzi 10 waliweza kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2023. Mwanafunzi wa kwanza Samson Apayo,47, alijizatiti na kuzoa alama 244,” alisema Askofu huyo.

Mchungaji wa Kanisa la Glory Outreach Assembly (GOA) akihutubu. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Tayari wanafunzi wapatao 40 wamejisajili kuendelea na masomo katika shule ya Noitan Adult School eneo la Turkana.

Askofu alisema hali ya maisha katika eneo hilo ni ngumu lakini walitumia ujuzi wao kuwahubiria wakazi hao na ndipo walipendekeza maswala ya kupata elimu licha ya kuwa watu wazima.

“Iwapo watu wazima watapata masomo hata kama ni ya kiwango cha chini, bila shaka watapata mawazo tofauti ya kuendesha mambo yao,” alifafanua mchungaji huyo.

Mchungaji huyo alisema haikuwa kazi rahisi kuwahamasisha wakazi hao wa Turkana kukumbatia masomo lakini uwezo wa Mwenyezi Mungu umezalisha matunda.

Alisema kanisa hilo litatuma wachungaji wengine kuwahamasisha wakazi wa Turkana umuhimu wa masomo.

Mwalimu mkuu katika shule hiyo Emmanuel Eyapan amepongeza juhudi za kanisa la GOA kuwaletea masomo nyumbani.

“Hatua hiyo inaendelea kuzaa matunda ambapo tukiendelea na kuwahamasisha watu wazima kuhusu umuhimu wa masomo, bila shaka tutafanikiwa pakubwa,” alifafanua mwalimu mkuu Bw Eyapan.

Alisema masomo ni muhimu kwa maisha ya binadamu kwa sababu humsaidia mja kubadilisha mtazamo wa mambo na kufikiri maswala ya maendeleo.

Mchungaji Mark Alibat alisema hatua ya Kanisa la GOA kuingiza masomo ya watu wazima Turkan imeleta mabadiliko makubwa ambapo wachungaji wataendelea kuombea wakazi hao kubadilisha mtazamo wao wa maisha.

“Tunaelewa uhasama wa kikabila wa kila mara ni jambo la hatari na ndiyo maana tunataka kumaliza kero hiyo kupitia masomo ya watu wazima,” alifafanua mchungaji Alibat.

  • Tags

You can share this post!

Krismasi: Wewe ndiye umesota! Wengine wanaponda raha

Ruto: Kenyatta aliacha ghala tupu hata panya walilitoroka

T L