• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
Mama na binti wakana kukwepa kulipa ushuru wa Sh2.2Bilioni

Mama na binti wakana kukwepa kulipa ushuru wa Sh2.2Bilioni

Na RICHARD MUNGUTI

BAADA ya kukwepa mtego wa polisi walipofumaniwa wakiwa mafichoni katika hoteli ya Weston inayomilikiwa na Naibu wa Rais William Ruto, mama na bintiye hatimaye walijisalimisha kwa korti jana kujibu mashtaka.

Bi Mary Wambui Mungai na bintiye Purity Njoki Mungai ni wakurugenzi wa kampuni ya Purma Holdings Limited inayowindwa na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) kwa kukwepa kulipa ushuru wa Sh2.2 bilioni. Wawili hao walijisalimisha mbele ya hakimu mkuu Felix Kombo, katika Mahakama ya Mlimani jijini Nairobi baada ya maafisa wa ujasusi kupata habari kwamba walilenga kutorokea nchini Zambia.

Kulikuwa na kizazaa katika Hoteli ya Weston Jumatano usiku baada ya maafisa wa polisi kuzingira mkahawa huo wa kifahari wakilenga kuwanasa washukiwa hao. Hata hivyo mama huyo na bintiye waliponyoka tena kutoka mle hotelini lakini polisi walifaulu kupata katika vyumba walivyokuwa wamekodi pasipoti ya Wambui ya kusafiri had nchini Zambia na Leseni ya bastola anayomiliki.

Polisi hawakuchoka ila waliondoka mle hotelini na kufululiza katika hospitali ya Nairobi Hospital ambapo Wambui alidai alikuwa amelazwa. Mle hospitalini hawakumpata Wambui na bintiye. Katika kile hakimu mkuu Felix Kombo alisema, “ulikuwa mchezo wa paka na panya polisi walienda katika makazi yao yaliyoko mtaa wa Mimosa jijini Nairobi. Hawakuwapata.”

Washtakiwa hao walijisalamisha mbele ya Bw Kombo anayesikiza kesi za ufisadi baada ya kuwaamuru wajisalamishe kwa mahakama Desemba 9,2021. Polisi walipata kibali cha kuwatia nguvuni mnamo Desemba 6,2021 lakini hawakufanikiwa kuwafikia.

“Polisi walipata habari za kijasusi kuwa wawili hao walikuwa wanatorokea Zambia. Habari zilisambazwa katika vituo vya mipakani na katika viwanja vya ndege nchini zikitoa ilani wawili hao wasiruhusiwe kuabiri ndege yoyote.” “Mnamo Desemba 8,2021 nilipokea habari za kijasusi kwamba wawili hao walikuwa wamejificha katika hoteli ya Weston.

Walikuwa wamekodisha vyumba nambari A301, A302 na B302,’’ afisa anayechunguza kesi hiyo alieleza mahakama. Hakimu alielezwa ni mfuko mweusi uliokutwa katika chumba nambari B302. Polisi walipoupekua walipata Kadi za Benki, Kitambulisho cha Kitaifa, Pasipoti ya Zambia, leseni ya umiliki wa silaha zote wa Wambui.

Polisi pia walienda Hospitali ya Kiambu Level-4 ambapo walipata habari Wambui alikuwa ameenda kupokea matibabu na kuagizwa apumzike nyumbani kwa siku tano. Mawakili Nelson Havi na Silvanus Osoro Onyienga aliyepia Mbunge wa Mugirano Kusini waliwasilisha maombi kadhaa kuanzia Desemba 6,2021 kupinga washtakiwa wasitiwe nguvuni lakini Bw Kombo akatupilia mbali ombi lao.

“Ikiwa washtakiwa wanataka kuwa na usalama na sheria wajisalamishe kortini Desemba 9,2021,” Bw Kombo alimweleza Bw Havi mnamo Desemba 8,2021. Wambui na bintiye Njoki walijisalamisha mbele ya Bw Kombo jana asubuhi kisha wakakanusha mashtaka manane ya kukwepa kulipa KRA ushuru wa Sh2.2bilioni kuanzia 2004.

Bi Thuguri alipinga wakiachiliwa kwa dhamana akisema tabia yao imezorotesha imani ya mahakama kwao. Lakini Bw Havi aliomba mahakama izingatie Wambui na Njoki walitii agizo la korti wajisalamishe Desemba 9,2021. Mahakama iliombwa iwaachilie kwa dhamana ya Sh5milioni pesa tasilimu.

Bw Havi alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa na hakuna sababu nyeti korti inaweza kutegemea kuwanyima dhamana. Lakini Bi Thuguri aliomba mahakama itilie maanani washtakiwa hao walikuwa wamekwepa polisi kusudi wasishtakiwe.

Akitoa uamuzi Bw Kombo alilaani tabia ya Wambui na Njoki ya kuwahepa polisi “badala ya kufika kortini kujibu mashtaka nane.” “Tabia ya wawili hawa kuwahepa polisi kwa lengo la kutoroka haikubailiki kamwe. Nailaani.Wangelifika kortini Desemba 6,2021 na kujibu mashtaka pata shika hii nyingi haingekuwa,” akasema Bw Kombo.

Hata hivyo hakimu alisema “wawili hao wamejiokoa kwa kujisalamisha kwa mahakama.” Hakimu aliwaagiza walipe dhamana ya Sh25miliioni pesa tasilimu kila mmoja. Wote wawili watawasilisha dhamana ya jumla ya Sh50milioni. Endapo watashindwa kulipa dhamana hiyo waliagizwa wawasilisha dhamana ya Sh50milioni na wadhamini wawili wa kiasi sawa na hicho.

Mbali na dhamana hiyo wawili hao waliagizwa wawasilishe pasipoti zao zote mahakamani.Pia waliamriwa wafike afisi za KRA Desemba 14,2021 kuchukuliwa alama za vidole. Kesi hiyo itatajwa Desemba 16,2021 kwa maagizo zaidi.

Wambui, Njoki na kampuni yao Purma Holdings Limited walishtakiwa kutolipa ushuru wa Sh2,231,789,125.

You can share this post!

Bifwoli apeperusha bendera ya Kenya vilivyo uogeleaji Uganda

Arsenal matumaini tele itajifufua ikipepetana na...

T L