• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Raila afichua ‘bonge la skendo’ kuhusu kile anadai ni kiini cha bei ya mafuta kuwa ghali nchini

Raila afichua ‘bonge la skendo’ kuhusu kile anadai ni kiini cha bei ya mafuta kuwa ghali nchini

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, sasa anataka mkataba wa ununuzi wa mafuta baina ya serikali ya Kenya na mataifa mawili ya Kiarabu ufutwe na waliohusika kuchunguzwa na kufutwa kazi serikalini.

Bw Odinga anasema mpango huo uliotangazwa na Rais William Ruto Aprili mwaka huu ni kashfa kubwa ambayo imechangia gharama ya juu ya maisha nchini.

Mnamo Aprili mwaka huu, Rais William Ruto alitangaza kuwa, serikali yake ilitia saini Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali ya Kenya na Saudi Arabia na Milki ya Kiarabu kuuzia Kenya mafuta kwa bei nafuu.

Ruto aliambia taifa kuwa, baadhi ya maafisa katika utawala wake walifanikiwa kuweka pamoja mpango ambao ungepunguza gharama ya mafuta nchini.

“Leo, tunaweza kununua mafuta kwa shilingi za Kenya, jambo ambalo watu wengi hawakuwahi kufikiria kuwa lingewezekana. Kwa kweli, katika muda wa mwezi mmoja ujao au zaidi, utaona kiwango cha ubadilishaji kikishuka kwa njia ya ajabu sana. Kwa makadirio yangu, katika miezi michache ijayo, kiwango cha ubadilishaji kitakuwa chini ya Sh120, hata kinaweza kuwa Ksh115,” rais alisema kuhusu mpango huo.

Lakini Raila anasema Kenya haikutia saini mkataba wowote na Saudi Arabia au UAE bali na kampuni za serikali za mafuta za petroli katika Mashariki ya Kati.

“Wizara ya Nishati na Petroli ilitia saini mkataba na kampuni za petroli zinazomilikiwa na serikali katika Mashariki ya Kati. Kwa nini Ruto alichagua kutambulisha mpango huo kama wa serikali kwa serikali? Hii ni ishara ya kwanza ya ufisadi katika mpango huu,” kiongozi huyo wa ODM alisema.

Bw Odinga alisema kubatiza mpango huo kuwa wa serikali kwa serikali kulikusudiwa kukinga kampuni tatu za Kenya kutokana na kulipa asilimia 30 ya ushuru wa kampuni.

Kulingana na Raila, mkataba huo haujashughulikia matatizo yoyote ambayo Ruto alisema yangeshughulikia.

“Gharama ya mafuta ilipanda hata zaidi baada ya mpango huo. Kwa nini hali imekuwa mbaya zaidi tangu mpango huo utangazwe?

Mpango huo ulikuwa ulaghai ambao sasa tunataka ufichuzi na uwajibikaji kamili. Ni kashfa kubwa,” alidai.

Raila aliitaka serikali kufutilia mbali kandarasi hiyo mara moja na kurejelea Mfumo wa Zabuni ya wazi ambao anasema ulihakikisha upatikanaji wa bidhaa za petroli kwa ushindani.

Pia anataka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi kuchunguza “kwa nini tuliingia katika mpango huu na nani ananufaika nao.”

Zaidi ya hayo, Raila anaomba shirika la kupambana na ufisadi kuhakikisha waliohusika wanalipa hasara waliyoingiza nchi na kufutwa kazi
Kiongozi huyo wa chama cha ODM alishangaa kwa nini gharama ya mafuta haijashuka tangu mkataba huo utiwe saini na kwa nini thamani ya shilingi ya Kenya imeendelea kudidimia dhidi ya dola.

“Ni wazi mpango huo haujashughulikia matatizo yoyote ambayo Ruto alisema ingeshughulikia. Ruto alipoanzisha mpango huu, kiwango cha ubadilishaji cha dola ya Amerika hadi shilingi ya Kenya kilikuwa Sh132. Leo, miezi sita baadaye, ni Ksh159 kwa dola. Gharama ya mafuta ilipanda sana baada ya mpango huo,” alisema.

“Tunamtaka Ruto kuchapisha mkataba huu. Hakuna anayejua jinsi Gulf Energy, Galana Oil Kenya Ltd na Oryx Energies Kenya Limited zilivyoteuliwa kushughulikia usambazaji wa humu nchini,” akasema.

Ili kupunguza gharama za juu za mafuta, alidai serikali lazima irejeshe ushuru wa ziada wa thamani hadi asilimia 8 kutoka asilimia 16 iliyoanzishwa na Sheria ya Fedha ya 2023.

“Serikali lazima itangaze hadharani kile inadai ni mkataba kati ya Kenya na Saudi Arabia na Milki ya Kiarabu na Wizara ya Nishati na Petroli lazima iweke hadharani makubaliano ambayo ilitia saini na kampuni za mafuta,” alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani.

Pia, anataka Wizara ya Nishati na Petroli kutangaza hadharani Mkataba wa Ununuzi iliyotia saini na kampuni za mafuta na EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai kuchunguza muundo wa bei wa kampuni hizo tatu za mafuta.

“Lazima Mamlaka ya Ushuru ya Kenya ijitokeze wazi na kueleza ni kwa nini zinawezeshwa kukwepa mabilioni ya ushuru huku Wakenya wa kawaida wakinyanyaswa kwa ushuru,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Akothee aliyeoga na kurudi soko, ametwaliwa tena na...

Madai ya Raila kuhusu skendo ya mafuta ni ‘hot...

T L