• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 1:20 PM
Ruto: Kuanzia 2024 hatutakuwa tukiagiza mahindi nje ya nchi, nimeweka mikakati kabambe kuboresha mazao

Ruto: Kuanzia 2024 hatutakuwa tukiagiza mahindi nje ya nchi, nimeweka mikakati kabambe kuboresha mazao

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto amesema mwaka ujao, 2024 utakuwa wa mwisho Kenya kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi.

Kiongozi wa taifa alisema haya alipohudhuria ibada ya Jumapili, Oktoba 29, 2023 katika Kanisa la Kianglikana Dayosisi ya Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Akisifu mpango wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, Rais alisisitiza kuwa lengo lake ni kuzima mchakato wa kuagiza mahindi kutoka ughaibuni kupitia upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima.

“Hatutaki kuagiza mahindi tena kutoka nje ya nchi. Mwaka ujao (2024) utakuwa wa mwisho kuagiza mahindi. Lakini kutoka 2025 tutazalisha mahindi yote hapa Kenya,” Rais alisema.

Uzalishaji wa kiwango kikubwa cha mazao ya shambani hutegemea sana utumizi wa mitambo na miundomsingi ya kiteknolojia.

Dkt Ruto alikiri changamoto hii kuwa kizingiti cha azma ya kuimarisha sekta ya kilimo nchini, lakini alisema atatoa suluhu.

“Nimeweka mpango kuanzia mwaka kesho kutakuwa na matingatinga ya kutosha kila sehemu Kenya. Mashamba yaliyoko kila mahali yanafaa kutumiwa kuzalisha chakula,” alisema akiona haya ya kutumia mashamba ya magereza na idara ya jeshi kuokoa gharama kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.

Hali kadhalika, Rais alitaka wakulima kukausha mahindi yao katika maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka (NCPB) kwa bei nafuu akilenga kudhibiti hasara baada ya mavuno.

Dkt Ruto alisema gharama ya kuanika mahindi sasa ni Sh70 badala ya bei ya awali ya Sh300 kwa kila gunia la kilo 90.

“Pia mkitaka kuhifadhiwa mahindi katika maghala ya NCPD, tutawatunzia kwa Sh10 kwa gunia kila mwezi ukiendelea kutafuta soko,” aliongeza, akisema wakulima hawajalazimishwa kuuzia serikali mahindi yao.

Wakulima tayari wamekataa bei iliyotangazwa na serikali ya Sh4, 000 kwa gunia la kilo 90, iliyotolewa na Wizara ya Kilimo.

  • Tags

You can share this post!

Mitihani ya KCPE 2023 na KPSEA yaanza kote nchini

Vijana Mombasa walalamikia kubaguliwa kuajiriwa kazi katika...

T L