• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Ruto, Raila kuvamia ngome ya Mudavadi juhudi za kumrai zikiendelea

Ruto, Raila kuvamia ngome ya Mudavadi juhudi za kumrai zikiendelea

Na DERICK LUVEGA

NAIBU Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga, wamepanga kuvamia ngome ya kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi ya Vihiga, huku madai yakienea kuwa kila mmoja wao anapanga kumvutia katika mrengo wake.

Dkt Ruto atakuwa akirejea Vihiga huku akitarajiwa kupiga kambi katika maeneobunge ya Sabatia, Vihiga, Emuhaya, Luanda na Hamisi.

Alizuru maeneo haya mara ya mwisho mnamo 2019.

Nao wandani wa Bw Odinga, watakuwa katika uga wa Hamisi wikendi hii, kuvumisha vuguvugu lao ambalo linajulikana kama Azimio la Umoja, ingawa duru zinaarifu kuwa waziri huyo mkuu wa zamani, hatahudhuria hafla hiyo kutokana na majukumu mengine.

Kwa mujibu wa Mshirikishi wa UDA katika Kaunti ya Vihiga, Bi Jackline Mwenesi, ambaye pia ni diwani maalum, Dkt Ruto atakuwa akitumia ziara hiyo kuwafafanulia wakazi kuhusu ajenda yake ya kuwainua maskini maarufu kama ‘Bottom Up’ na pia kumwinda Bw Mudavadi.

Mnamo 2019, Dkt Ruto akiwa katika eneo hilo, alimwomba Bw Mudavadi aunge mkono azma yake, ombi ambalo waziri huyo mkuu wa zamani alikataa, akisema Naibu Rais ana doa la ufisadi na hawawezi kushirikiana naye kisiasa.

“Naibu Rais atahutubia mikutano ya hadhara katika maeneobunge yote matano ya kaunti hii kisha kushiriki hafla za michango ya kuinua makundi mbalimbali ya vijana, akina mama na wazee. Pia atamrai Bw Mudavadi ajiunge na chama hicho kwa kuwa UDA ndiyo jukwaa bora la kuhakikisha anasalia kwenye siasa za kitaifa,” akasema Bi Mwenesi.

Mkutano wa Azimio la Umoja utakaoandaliwa Jumapili nao unatarajiwa kuvumisha ODM zaidi katika kaunti hiyo na unajiri wiki chache baada ya mbunge maalum wa ANC, Bw Godfrey Osotsi, kusema analenga kiti cha Useneta kwa kutumia chama hicho.

Bw Osotsi anatarajiwa kuuza ajenda zake kwenye mkutano huo utakaohudhuriwa na mbunge wa Luanda, Bw Chris Omulele wa ODM pamoja na mwaniaji wa kiti cha ubunge cha Hamisi kupitia chama hicho, Bw Castro Khabongo.

“Mkutano huo umepangwa na vijana na wasomi wa Vihiga. Binafsi nitahudhuria japo sina uhakika iwapo Bw Odinga atahudhuria. Ingawa hivyo, tuna viongozi wengi kutoka maeneo mbalimbali ambao watahudhuria,” akasema Bw Osotsi.

Huku Dkt Ruto na Bw Odinga, wote wakimng’ang’ania Bw Mudavadi, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Vihiga Beatrice Adagala na mbunge wa Sabatia Alfred Agoi, wamesema kuwa kiongozi huyo wa ANC atafika debeni na hawezi kumuunga yeyote 2022.

“Tunawaomba watu wetu wasalie nyuma ya Bw Mudavadi kwa sababu umaarufu wake unazidi kupanda na ndiye ataongoza muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kubuni serikali,” akasema Bw Agoi.

You can share this post!

Jambazi aua mwenzake kwa kisu kimakosa, 2 waangushwa na...

Covid: Kagwe aapa kupuuza uamuzi wa korti kuhusu chanjo

T L