• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Covid: Kagwe aapa kupuuza uamuzi wa korti kuhusu chanjo

Covid: Kagwe aapa kupuuza uamuzi wa korti kuhusu chanjo

RICHARD MUNGUTI na PIUS MAUNDU

MAHAKAMA Kuu imepiga breki agizo la Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwamba Wakenya ambao hawatakuwa wamepata chanjo dhidi ya Covid-19 kufikia Desemba 21 hawatapata huduma muhimu.

Lakini Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema hawatasitisha uamuzi wa kuwanyima huduma muhimu watu ambao hawajapata chanjo.

Jaji Antony Mrima alisitisha kutekelezwa kwa agizo hilo hadi kesi iliyowasilishwa na mfanyabiashara Enock Aura isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji Mrima alisema agizo hilo linakandamiza haki za wananchi ikitiliwa maanani sio wote wanaweza kupata chanjo hilo kufikia Desemba 21, 2021.

Jaji huyo alisema kuwa kesi aliyowasilisha Bw Aura akihoji masuala chungu nzima kuhusu uhalali wa agizo hilo, iko na mashiko kisheria na inafaa kusikizwa kwa mapana ili uamuzi utakaofaidi kila mtu utolewe.

“Baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na wakili Harison Kinyanjui, kuna ushahidi wa kutosha kwamba agizo la Bw Kagwe lapaswa kusitishwa,” alisema Jaji Mrima.

Mahakama iliamuru washtakiwa wawasilishe majibu katika muda wa siku 14.

Jaji Mrima aliratibu kesi hiyo kuwa ya dharura.

Katika kesi hiyo, Bw Aura amewashtaki mawaziri wa afya, uchukuzi, ujenzi miongoni mwa wengine.

Bw Kagwe alitoa agizo hilo Novemba 2021 akiamuru Wakenya ambao hawatakuwa wamepokea chanjo hiyo kufikia Desemba 21, 2021 wasipewa huduma zikiwemo za serikali.

Bw Aura alisema agizo hilo linawaathiri wananchi wengi na wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na sekta ya uchukuzi.

Mahakama ilielezwa wahudumu wa matatu wanaojiandaa kuwasafirisha wananchi kutoka maeneo ya mijini hadi mashambani Krismasi wataathirika pakubwa.

You can share this post!

Ruto, Raila kuvamia ngome ya Mudavadi juhudi za kumrai...

Akina dada 500 wakongamana Thika kupewa hamasisho la...

T L